Lyamungo, Umbwe sasa chini ya ulinzi
Polisi mkoani Kilimanjaro imeendelea kuimarisha ulinzi katika shule za Umbwe na Liyamungo zilizopo Wilaya za Moshi na Hai baada ya kutokea vurugu kubwa zilizosababisha mwanafunzi mmoja kufariki dunia na wengine sita kujeruhiwa vibaya.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana shuleni humo na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Lucas Ng’hoboko, ulinzi huo utaimarishwa hadi hapo hali ya amani na utulivu utakaporejea.
Hata hivyo, zipo taarifa kuwa baadhi ya wanafunzi wa shule hizo wamekuwa wakihojiwa kuhusiana na matukio hayo na kwamba polisi wanaendelea kuchunguza chanzo cha vurugu hizo na mauaji hayo.
Hata hivyo, serikali wilayani Moshi imesema imesikitishwa na tukio hilo kwani kwa namna moja au nyingine linarudisha nyuma jitihada za serikali katika kuboresha elimu kwani vurugu hizo zimesababisha hasara ya mamilioni ya fedha.
Mkuu wa wilaya hiyo, Mussa Samizi, alisema ni vyema wanafunzi wakaishi mashuleni kwa kufuata kilichowapeleka kwani elimu wanayoipata ni kwa faida yao.
Vurugu hizo zilizotekea alfajiri ya Agosti 22, mwaka huu, zilisababisha wanafunzi wa Shule ya Sekondari Umbwe, Ayoub Talaka (19) wa kidato cha tano na mkazi wa Mkoa wa Mbeya, kupoteza maisha na wengine watatu kujeruhiwa.
0 comments:
Post a Comment