TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU / ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT CHEAP RATES | CONTACT ME: kilinyepesi@gmail.com

 photo DTB_zps7bd2662d.jpg

 photo fl_zps09337f7a.jpg


Habari Mpya:
Friday, August 14, 2009

Jane Mweni ashinda Faidika na BBC!

12:01 PM
Mwanadada Jane Mweni ameibuka mshindi wa shindano la Faidika na BBC baada ya kuwabwaga wenzake watano kwenye fainali iliyofanyika katika jiji la Mombasa, Pwani ya Kenya.

Mchanganuo wake wa kuanzisha mradi wa kuzoa takataka katika jiji la kitalii la Mombasa ndiyo ilikuwa siri ya ushindi kwa Bi Mweni mwenye umri wa miaka 21 ambaye aliwasilisha mchanganuo wake kwa kujiamini na ufasaha.

Akipokea zawadi ya dola 5,000 za Marekani na kikombe, Jane alisema ameishiwa maneno: "Nashindwa kuzungumza...." huku akibainisha kuwa anajihisi mwili wake umeishiwa nguvu kwa furaha ya kuibuka mshindi.

Bi Mweni ni mkazi wa Mombasa, kwa sasa anasema alikuwa akisubiri matokeo ya mitihani ya diploma aliyoifanya hivi karibuni.

Kijana Mbaraka Juma kutoka Tanzania aliambulia nafasi ya pili kutokana na mchanganuo aliowasilisha wa kutaka kuanzisha biashara ya kufuga vyura na panya vitakavyotumika na shule za msingi na sekondari pamoja na taasisi za elimu ya juu kufanya utafiti wa kisayansi.

Mwanadada mwingine Nyota Anjelique kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alimaliza katika nafasi ya tatu akiwa amelenga biashara ya mafuta ya mawese.

Shindano la Faidika na BBC lilianzishwa mwaka 2007, limekuwa kila mwaka likiwapambanisha vijana kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati kumpata mmoja wao mwenye kipaji cha ujasiriamali.

Mwaka huu mshindi amezawadiwa dola 5,000 za Marekani, kikombe na fursa ya kuhutubia katika kongamano la vijana kwenye mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Madola huko Trinidad and Tobago mwezi Novemba 2009.

Washindani wengine walikuwa Chiza Bonye wa Burundi, Hakizimana Aladin aliyeiwakilisha Rwanda na Gakuo Roy wa Uganda.



0 comments:

Post a Comment

 
BONYA HAPA