.jpg)
Wanafunzi Jijini Dar es Salaam, Pwani na kwingineko nchini wametakiwa kujiepusha na vitendo vya wizi wa mitihani na badala yake wazingatie zaidi masomo ili waelewe na hatimaye waweze kufanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho.
Wito huo umetolewa na Mkaguzi wa Shule za Sekondari, Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Catherine Baybit, wakati akizungumza kwenye mahafali ya nane ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Ujenzi iliyopo Mkuranga mkoani Pwani.
Mkaguzi huyo akasema kuwa siku zote, wanafunzi wanapaswa kuongeza juhudi katika masomo yao na kwamba baada ya hapo, watakuwa na uelewa mkubwa utakaowafanya watembee na majibu ya mitihani vichwani mwao.
"Majibu ya mitihani yapo katika yale mliyofundishwa darasani na kisha wenyewe mkajisomea zaidi na kuyashika vichwani mwenu... jipangeni kiakili na mtaweza kukumbuka yote, wala hampaswi kuwa na hofu," akasema Bi. Catherine.
Aidha, Mkaguzi huyo akasema suala la kurejeshwa kwa michepuo shuleni limeshaanza kufanyiwa kazi na Serikali.
Amesema hatua hiyo iliyoanza kuchukuliwa na Serikali ina lengo la kuwawezesha wahitimu kuwa na ujuzi utakaowafanya wamudu vyema harakati za maisha baada ya kumaliza masomo yao.
Mkaguzi huyo ametoa maelezo hayo baada ya kusikia rai toka kwa uongozi wa shule hiyo, juu ya umuhimu wa kurejeshwa kwa shule za michepuo maalum.
Katika hatua nyingine, uongozi wa shule hiyo ya Ujenzi ambao pia unamiliki shule za St. Mark's na St. Mathew's, umewaasa wanafunzi wake Waislamu kuzingatia ibada inayoendelea sasa ya funga ya Ramadhani kwa vitendo.
Mkurugenzi wa shule hizo, Bw. Thadeus Mutembei, amesema uongozi wao utatekeleza vyema jukumu lake la kuwapatia futari, daku na huduma nyingine wanafunzi wanaoendelea na ibada hiyo, kwa kuamini kuwa hatua hiyo ya kuwa huru kutekeleza imani yao itawafanya waendelee kuzingatia vizuri masomo yao ya darasani.
0 comments:
Post a Comment