Mjamzito afia kwenye benchi hospitalini Dar
Mwanamke mmoja mjamzito anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 25 na 30 amefariki dunia akiwa amekaa kwenye benchi la hospitali moja Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Sebastian Masinde amesema tukio hilo la kusikitisha lilitokea jana mishale ya saa 3:00 asubuhi katika zahanati iitwayo M.Tatu, iliyoko Mwananyamala Kisiwani.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Masinde amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mama huyo alikwenda kwenye zahanati hiyo akiwa mgonjwa mahututi, huku akiwa hawezi hata kuzungumza vizuri.
Akasema baada ya kumchunguza, madaktari waligundua kuwa alikuwa na ujauzito usipungua miezi sita na pia alikuwa na upungufu wa damu.
Akasema kutokana na hali yake ilivyokuwa, madaktari hao wakamshauri mwanamke huyo aende hospitali ya Serikali ambako angeweza kupata huduma nzuri zaidi.
Kamanda Masinde akasema baada ya kushauriwa hivyo, mwanamke huyo alikwenda kujilaza kwenye benchi ambako alifariki.
Amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mwananyamala na kuwa Polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi juu ya kifo hicho.
0 comments:
Post a Comment