KUTEKWA, kupigwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chama cha
Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka na hatimaye kufungiwa kwa Gazeti
la MwanaHalisi kwa muda usiojulikana, kumeleta kizaazaa katika kampuni
ya simu za mkononi ya Tigo, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Habari kutoka ndani ya kampuni hiyo ya simu yenye mtandao mpana
nchini, zinasema kuwa zaidi ya wafanyakazi 30 wamefukuzwa kazi na
wengine wako kwenye uchunguzi wakituhumiwa kuvujisha mawasilino ya siri
ya simu za wateja kwa Gazeti la MwanaHalisi.
Kwa mujibu wa habari hizo, taarifa za mawasiliano za simu zinazodaiwa
kuvujishwa na wafanyakazi hao, zilikuwa kati ya Dk. Ulimboka, Afisa
Usalama wa Ikulu na watu aliowasiliana nao kabla ya kutekwa.
Rais Jakaya Kikwete amepata kuliambia taifa mara mbili kwa njia ya
televisheni, mwishoni mwa Juni na alipozungumza na wahariri wa vyombo
vya habari wiki iliyopita, kwamba serikali yake haihusiki kuteka, kutesa
na kumtupa daktari huyo porini.
Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda amepata kuliambia Bunge kuwa, serikali
yake haihusiki na utekaji, utesaji na kuhoji, “...serikali imteke ili
iweje?”
Hivi karibuni serikali ililifungia Gazeti la MwanaHalisi baada ya
kuandika habari iliyomtaja ofisa mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa
Ikulu (TISS), kuwa ndiye aliyetekeleza mpango wa kumteka, kumpiga na
kumtesa hadi kumjeruhi Dk. Ulimboka, ambaye kwa sasa anaendelea na
matibabu kwenye hospitali moja nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa habari hiyo ambayo serikali inadai kuwa ni ya uchochezi,
MwanaHalisi ilianika namba ya simu ya ofisa huyo pamoja na watu wengine
wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo linaloendelea kuchunguzwa na
kamati maalumu iliyoundwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai
(DCI).Endelea.>>>
0 comments:
Post a Comment