TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
YAH; UPOTOSHAJI WA ZIARA ZA CHAMA MIKOANI
Toka tarehe 03/05/2012 nimekuwa na ziara kadhaa za kichama
katika mikoa mbalimbali kwa lengo la kukiimarisha Chama. Baadhi
ya mikoa niliyofanikiwa kufika ni pamoja na Ruvuma, Njombe,
Iringa,Mbeya,Kagera,Rukwa na Katavi. Ziara hizi zimekuwa zikilenga
kufanya yafuatayo kati ya mengi niliyofanya:
Kukagua uhai wa Chama
Kukagua maendeleo ya uchaguzi ndani ya Chama
Kukagua miradi mbalimbali ya kiuchumi ya Chama
Kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM
Kwa muda sasa pamekuwa na juhudi za makusudi za kupotosha nia na
madhumuni ya ziara hizi na kujaribu kuonyesha kuwa kinachofanyika
hakina baraka za Chama na hivyo kimesababisha mgogoro ndani ya Chama,
hasa kati yangu na Katibu Mkuu.
Juhudi hizi zimelenga kukatisha tamaa jitihada mbalimbali zinazofanywa
na Chama za kuwa karibu na wanachama wake na wananchi. Kwa bahati
nzuri vyombo vya habari vinavyotumika kusambaza uzushi na uongo
huu vinajulikana ni vya nani, hivyo ni rahisi kujua kwanini wanafanya
wayafanyayo.
Kwa mfano, wanadai kuna pesa nyingi ninapewa mimi kama Katibu wa
Itikadi na Uenezi na ninapewa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM bila
Baraka za Katibu Mkuu wangu ambaye ndiye msimamizi wangu mkuu na
kwamba hilo limezua malalamiko na migongano kati yetu.
Huu ni uzushi wa kitoto sana, kwani wanataka kuwaaminisha wana CCM
na wananchi kwa ujumla kuwa mambo si shwari ndani ya CCM. Huku
wakipuuza ukweli kuwa Katibu Mkuu wa CCM ndo msimamizi wa mapato
na matumizi yote ya CCM, hivyo kama kuna ziara au jambo linalohusu
matumizi ya pesa ndani ya Chama, lazima liwe na baraka zake.
Lakini wanafumba macho ili wasione kuwa, Katibu Mkuu wa CCM ndio
mwenyekiti wa sekretarite ya Chama Taifa, hivyo sisi wajumbe wote wa
sekretarieti tunafanya kazi chini ya maagizo na usimamizi wake wa karibu.
Kama kuna mafanikio yeyote basi mwasisi wa mafanikio hayo ni Katibu
Mkuu wa CCM Taifa ndugu Wilson Mukama, kwani yeye ndiye kiongozi
wa sekretarieti hii.
Itakumbukwa kuwa nilipoanza ziara hizi, wapotoshaji hawa walituhumu
ziara zangu kuwa zinalengo la kutisha baadhi ya watu wasigombee nafasi
mbalimbali ndani ya Chama kisa wao na mimi tuna mitazamo tofauti ndani
ya chama. Nilipowataka kulithibitisha hilo na wakashindwa, sasa wamekuja
na tuhuma mpya.
Nawaomba wana CCM, wapenzi na mashabiki wa CCM na wananchi
kwa ujumla kuupuuza uongo na uzushi huu kwani hauna ukweli wowote.
Umetungwa na watu wenye roho mbaya wasioitakia mema CCM,
wanaotamani kuona CCM haitulii na hivyo mambo yasimame ndio furaha
yao. Sasa wakiona mambo yanakwenda viroho vyao vinawauma.
Nataka niwathibitishie sekretarieti ya Taifa ya CCM iko imara, thabiti,
madhubuti na yenye mshikamano tukifanya kazi kwa pamoja na upendo
chini ya uongozi imara wa Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Mukama.Wanao
yatunga na kuyasambaza haya wanapoteza muda wao.
Nawathibitishia uzushi huu hauta athiri kasi yetu ya kujenga Chama chetu
wala ari yangu binafsi katika kukitumikia Chama changu kwa nguvu zote.
Hivi ninavyoongea tayari maandalizi yamekamilika ya mkutano mkubwa
wa hadhara mjini Kigoma siku ya kesho tarehe 19/07/2012 kwa lengo la
kuzungumza na wana Kigoma juu ya mafanikio na changamoto mbalimbali
zinazoukabili mkoa wa Kigoma.
Katika mikutano hii mingi nina ambatana na baadhi ya mawaziri wa wizara
mbalimbali zenye maeneo ya utekelezaji kwenye mikoa husika. Kwa mfano
Kigoma tutazungumzia hatua iliyofikiwa katika sekta ya Uchukuzi kwa
maana ya reli, bandari na anga. Lakini mkoa huu una kero kubwa ya maji
hasa mjini Kigoma. Kuna changamoto kadhaa kwenye serikali za mitaa,
kuna mengi yanayoendelea ya ujenzi wa miundimbinu kama barabara nk.
Staili hii tunayotumia kwenye mikutano mingi ya hadhara ambayo kwakweli
inatutofautisha sisi Chama tawala na vyama vingine vya saisa nchini,
tuliizindua pale jangwani kwenye ule mkutano mkubwa wa kihistoria mwezi
Mei mwaka huu! Staili hii imepewa jina la AHADI NI DENI. Hivyo wana
Kigoma na maeneo mengine kaeni mkao wa kula, AHADI NI DENI inakuja
kwenu.
Itakumbukwa tuliwaahidi katika mkutano wa Jangwani kuwa tutazunguka
nchi nzima, lakini tofauti na wenzetu wanaotukana na kukashifu kila
kinachofanyika na kilichofanyika sisi tunakwenda kupeleka majawabu ya
changamoto mbalimbali kwenye maeneo yao. Na hii ndio tofauti ya vyama
vya upinzani na Chama tawala. Wakati wao wanabeba matusi na kejeli
kwenye mikutano yao, sisi tunabeba majawabu namtumaini kwa wananchi.
Kwahiyo “ahadi ni deni” imelenga kuzipitia ahadi zetu kwa wananchi na
namna spidi ya utekelezaji wake ilivyo.
Nawataka sasa, hawa wanaozusha maneno na kujaribu kupotosha ziara
nizifanyazo mikoani kuacha mara moja, kwani kukaa kwangu kimya haina
maana kuwa siwafahamu. Nawaonya wakiendelea nitawasema hadharani
bila kumumunya maneno. Nasema inatosha, upotoshaji mliofanya unatosha,
sasa basi.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na;
Nape Mose Nnauye
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM
Itikadi na Uenezi |
0 comments:
Post a Comment