MVUTANO mkali unadaiwa kuibuka katika kikao cha Kamati ya Siasa ya CCM mkoani Arusha baada ya baadhi ya wajumbe kupinga uongozi wa chama hicho Wilaya ya Arumeru, kumpitisha Sioi Sumari kugombea Ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki.
Chanzo cha habari ndani ya kikao hicho kilichoanza saa 5:00 asubuhi hadi saa moja usiku juzi, zinadai kuwa kitendo cha kupitishwa kwa jina la Sumari ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo marehemu Jeremiah Sumari, kimeibua malumbano makali ndani ya chama hicho.
Habari hizo zimeeleza kuwa wajumbe wawili waliokuwa katika kikao hicho ambao ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo na Katibu wa CCM mkoani Arusha Mary Chatanda, walipinga kupitishwa jina la Sumari, kwa sababu ushindi wake umelalamikiwa kila kona.
Taarifa zimedai kuwa kitendo cha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira kuhudhuria kikao hicho kama msikilizaji, kimezua utata baada ya baadhi ya wajumbe kuhoji ugeni wake ndani ya kikao hicho cha maamuzi ya chama.
Baadhi ya wajumbe waliokuwa wakipinga kupitishwa jina la Sumari, wametaja sababu iliyowafanya kutopitisha jina hilo kwa kutoa hoja kwamba ushindi wake umegubikwa na malalamiko mengi, hususan madai ya rushwa.
“Mkuu wa Mkoa pamoja na Chatanda ndio walikuwa wakipinga kupitishwa kwa jina la Sioi kulikuwa na mvutano mkali sana, lakini hadi dakika ya mwisho kikao kilipitisha majina ya watu wawili ambao ni Sioi na Sarakikya,” kilisema chanzo chetu. Hata hivyo, mvutano huo unasemekana kukiweka CCM katika wakati mgumu katika harakati za kutetea jimbo la Arumeru Mashariki ambapo kwa sasa makundi mawili, yameonekana kuvutana rasmi ambapo moja linaunga mkono jina la Sioi kupitishwa huku lingine likipinga.
Baadhi ya wanachama wa CCM mkoani Arusha wamekosoa utaratibu uliotumika kupitisha majina mawili (Sumari na William Sarakikya) ambayo yatapelekwa katika ngazi za juu kwa uamuzi wa mwisho wakisisitiza kwamba lililopaswa kupitishwa jina moja.
Wanachama hao bila kutaja majina yao, wamepinga vilevile kitendo cha Wassira kuhudhuria kikao hicho kama msikilizaji huku wakisema, kiongozi huyo hakustahili kuhudhuria kikao hicho kama msikilizaji kwa vile kilikuwa kikao cha maamuzi.
|
0 comments:
Post a Comment