TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU / ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT CHEAP RATES | CONTACT ME: kilinyepesi@gmail.com

 photo DTB_zps7bd2662d.jpg

 photo fl_zps09337f7a.jpg


Habari Mpya:
Thursday, February 10, 2011

WANAFUNZI 1200 WASIMAMISHWA MASOMO UDSM

8:17 PM
Mlimani wafukuza 1,200
Teofilo Mbeya watimua 508
Tumaini FFU watanda
Mkwawa mgomo kwenda mbele

Migomo ya vyuo vikuu nchini imeendelea kushika kasi na safari hii Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, sehemu ya Mlimani kimelazimika kuwasimamisha masomo wanafunzi 1,200 wanaosoma shahada ya kwanza katika Chuo ya Uhandisi na Teknolojia kwa kusababisha vurugu chuoni hapo.

Wakati hayo yakitokea jijini Dar es Salaam, mkoani Iringa nako Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (Teku), kimewasimaisha wanafunzi 508 kwa madai ya kusababisha vurugu huku polisi wakitawanya maandamano ya Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa (IUCO), waliokuwa wakitaka kwenda kwa Mkuu wa Mkoa kuomba kibali cha kwenda Dodoma kumuona Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Wanafunzi 1,200 waliosimamishwa katika Chuo cha Uhandisi Dar es Salaam wanadaiwa kufanya vurugu na kuwatisha wahadhiri kwa lengo la kuushinikiza uongozi wa chuo hicho umrudishe chuoni mwanafunzi mwenzao wa mwaka wa tatu, Jamson Babala, aliyefukuzwa baada ya kukutwa akiibia majibu ya mtihani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema wanafunzi hao wamesimamishwa kwa muda usiofahamika hadi hapo watakapotangaziwa.

Profesa Mukandala alisema hatua ya kuwasimamisha wanafunzi hao imefuatia kitendo chao cha kukaidi agizo lililotolewa la kuwataka waache vurugu.

“Vurugu hizi zilianza Ijumaa iliyopita ambapo kikundi cha wanafunzi wa Koleji hii wamekuwa wakivuruga madarasa na kuwatisha wahadhiri ili kushinikiza kurejeshwa chuoni mwanafunzi Babala ambaye tumemfukuza kwa kuangalizia mitihani,” alisema Mukandala.

Profesa Mukandala alisema Babala alikutwa na kosa hilo Novemba 12 mwaka jana wakati wa mitihani ya marudio.

Alisema baada ya msimamizi wa mitihani kumkamata na kumtaka ampe karatasi hiyo, mwanafunzi huyo alikataa kuisalimisha na badala yake aliiweka mdomoni na kuimeza.

Profesa Mukandala alisema Desemba 9, mwaka jana suala hilo lilifikishwa katika Kamati ya Masomo ya Shahada ya awali ambapo mtahiniwa pamoja na msimamizi wa mtihani husika walihojiwa.

Alisema katika kikao hicho, Babala alikiri kumeza karatasi ambayo aliielezea kuwa haikuwa na kitu chochote kinachohusiana na mtihani.

Alisema wasimamizi wa mitihani walipohojiwa, walieleza kuwa siku ya tukio kabla ya kuwaruhusu wanafunzi kuingia kwenye chumba cha mtihani, walikagua ili kuhakikisha hakukuwa na karatasi ya kitu kingine kinachoweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa taratibu za mitihani.

“Kutokana na majibu ya mtahiniwa na ushahidi wa watahiniwa wawili waliohojiwa, Kamati iliona ana hatia hivyo ikapendekeza kwa Seneti ya chuo aachishwe masomo kadiri ya maelezo ya kanuni za mitihani,” alisema.

Alisema Desemba 15 mwaka jana Seneti hiyo ya chuo ilijadili suala hilo kwa kina na ilikubaliana na pendekezo hilo na kupitisha uamuzi wa kumwachisha masomo wanafunzi huyo.

Alisema baada ya kufukuzwa, mwanafunzi huyo aliomba apunguziwe adhabu akidai kuwa wastani wa matokeo yake ya mitihani iliyopita ni wa kuridhisha.

Profesa Mukandala alisema kufuatia kanuni za mitihani na sheria nyingine, ombi hilo halikukubaliwa.

“Wanafunzi wameendelea kuvuruga masomo na kuhatarisha usalama wa watu na mali katika Koleji hii, leo (jana) wamemjeruhi mwanafunzi mwenzao kutokana na kukaidi kile walichokuwa wakitaka afanye,” alisema.

Alisema katika kikao cha dharura kilichofanyika juzi na kuhusisha Baraza la chuo, liliagiza ikiwa vurugu hizo zitaendelea masomo ya shahada ya kwanza katika Koleji hiyo yasimamishwe na wanafunzi husika waondolewe chuoni hapo.

Alisema hatua waliyoifikia ya kuwasimamisha masomo wanafunzi hao, ilifikiwa baada ya vurugu hizo kuendelea jana ambapo wanafunzi walifunga geti la kuingilia chuoni hapo kuwazuia wenzao pamoja na wahadhiri kuingia.

Akizungumzia tatizo la kuwepo kwa mgomo chuoni hapo, Profesa Mukandala alisema mara zote kila mgomo hutokea ukiwa na sababu zake ambapo mwaka 2007 na 2008 wanafunzi walikuwa wakilalamikia viwango vya mikopo pamoja na mikopo yenyewe.

Alisema tatizo hilo serikali imeanza kulishughulikia kupitia tume iliyoundwa kuchunguza Bodi ya Mikopo.

Alisema wakati wanafunzi hao wakiwa majumbani, uchunguzi wa kuwabaini vinara wa mgomo utakuwa ukifanyika.

Jana asubuhi NIPASHE ilishuhudia baadhi ya wanafunzi wa Koleji hiyo wakiwa wamefunga geti la kuingilia chuoni hapo.

Hata hivyo, baadhi ya wanafunzi waliozungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina, walisema wamesikitishwa na uamuzi huo na kuomba chuo kiwafikirie.

Wengine waendelea na masomo

Wakati huo huo, wanafunzi wa chuo hicho waliokuwa wakigoma ili kuushinikiza uongozi wao uwakopeshe Sh. 100,000 au chini ya hapo wameendelea na masomo.

508 WASIMAMISHWA KISANJI MBEYA

Nako katika Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (Teku) mkoani hapa hali inazidi kuwa mbaya ambapo chuo kimewasimamisha masomo wanafunzi 508, kutokana na vurugu walizozifanya kwa siku tatu mfululizo na kusababisha jana wapambane na Polisi wakati wakiandamana bila kibali.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Tuli Kassimoto, aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa chuo kimefikia hatua hiyo ili kumaliza mgomo ambao umesababisha masomo kusimama kwa siku tatu mfululizo.

Alisema baada ya wanafunzi hao kuendesha mgomo kwa siku tatu mfululizo, jana Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, aliukutanisha uongozi wa Chuo hicho pamoja na serikali ya wanafunzi na kufikia makubaliano ya kuwarejesha wanafunzi hao nyumbani ili kudhibiti usalama chuoni hapo.

Hata hivyo, Profesa Kassimoto alisema wanafunzi hao wote watarejeshwa shuleni kwa kufuata taratibu za chuo hicho na kuwa uchunguzi zaidi juu ya mgomo huo bado unaendelea.

Alisema baada ya uchunguzi kumalizika, wanafunzi watakaobainika kuwa walikuwa vinara wa mgomo huo, watachukuliwa hatua za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kufukuzwa chuoni hapo.

Akizungumzia chanzo cha mgomo huo, Profesa Kassimoto alisema wanafunzi wa mwaka wa tatu wanaosoma somo la Historia ndio walioanza kumkataa mmoja wa wahadhiri wao kwa madai kuwa mhadhiri huyo alikuwa akiwaporomoshea matusi ya nguoni.

Alisema baada ya malalamiko hayo kuufikia uongozi wa Chuo, hatua zilichukuliwa haraka, ikiwa ni pamoja na kumsimamisha mhadhiri huyo na kumwondoa kabisa asiendelee kufundisha chuoni hapo.

Alisema hata hivyo, uongozi wa Chuo ulikuwa bado haujawataarifu wanafunzi juu ya hatua zilizochukuliwa na kuwa ndio sababu wanafunzi hao waliamua kugoma.

Alisema wakati mgomo huo ukianza, Msaidizi wa Makamu wa Chuo aliamua kwenda kuzungumza na wanafunzi hao, lakini walikataa kumsikiliza, na hata Makamu Mkuu wa Chuo alipokwenda kuzungumza nao tayari walikuwa wamepandwa na jazba na kuanza maandamano.

“Tatizo lilikuwa ni la mawasiliano baina ya utawala na wanafunzi, na baada ya hali kuwa mbaya wanafunzi hawakutaka kumsikiliza mtu yeyote na ndio sababu hali ilikuwa vile, lakini kama wangekubali kumsikiliza mkuu wa Chuo wasingeandamana kwa sababu alitaka kuwaeleza kile wanachokitaka,” alisema Profesa Kassimoto.

Alisema ili wanafunzi waliosimamishwa masomo warejeshwe chuoni, wanatakiwa kuandika barua ya kuomba kurudi na kisha watatakiwa kujaza fomu maalumu za kujiandikisha upya chuoni hapo.

MGOMO WA IUCO IRINGA

Polisi mkoani Iringa, wameyazuia maandamano ya wanafunzi wa IUCO waliokuwa wakiandamana bila kibali kwenda kumuona Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa lengo la kupewa kibali cha kwenda mkoani Dodoma kumpelekea kilio chao Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Wanafunzi hao wa mwaka wa kwanza wanaosoma Shahada ya Elimu katika Sanaa, walikumbana na kizingiti hicho mita chache kabla ya kufika lango kuu la kuingilia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Wakiwa wanaelekea katika ofisi hiyo wakitembea kwa miguu na wengine wakiwa wamepanda katika mabasi madogo ya kukodi, Polisi waliokuwa katika gari aina ya Toyota Pick Up Land Cruiser) lenye namba PT 1909 walilizuia kundi hilo na kuwaamuru wanafunzi hao kutawanyika kwa hiyari yao kabla ya kutumia nguvu.

“Haloo, hapa mwisho, wote rudini nyuma na muelekee chuoni kwenu, kwanza hamna kibali cha kuandamana, msitulazimishe tutumie nguvu za ziada kwani mnakwenda wapi …

“Kama mnataka chagueni wawakilishi wawili tu ili wakawawakilishe huko, lakini wengine tuondoke eneo hili haraka,” alisema kiongozi mmoja wa askari hao aliyeamuru kutoendelea kwa maandamano hayo.

Dakika chache baadae, ujumbe wa wanafunzi wawili ukioongozwa na Likinjiye Ole Mollel na Juma Malendeja, uliteuliwa kwenda kumuona Mkuu huyo wa Mkoa ili kumweleza yaliyowatokea baada ya uongozi wa chuo hicho kushindwa kuisajili kozi hiyo katika Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU).

Alipohojiwa na gazeti la NIPASHE, mmoja wa wanafunzi hao, Likinjiye Ole Mollel, alisema kuwa nia yao ya kwenda kwa Mkuu wa Mkoa ni kumweleza tatizo lao na kumwomba awape kibali ili waende mkoani Dodoma kuonana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wamweleze shida yao.

Wanafunzi hao wanalalamikia chuo hicho kushindwa kuisajili kozi ya elimu upande wa sanaa TCU.

Wakati tukio hilo likitokea karibu na ofisi ya Mkuu huyo wa Mkoa, askari wa FFU, waliokuwa na magari matatu, walikuwa ndani ya eneo la Chuo Kikuu cha Tumaini wakihaha kuzuia zisitokee vurugu kutokana na mgomo huo.

Mapema jana asubuhi, wanafunzi hao walifunga barabara ya Tumaini kupitia Sentema hadi Tumaini na baadae askari wa FFU waliwatangazia kwamba wangetumia nguvu kama wasipoondoka barabani, agizo ambalo walitii na kutawanyika.

Hata hivyo, ujumbe wa wanafunzi hao waliokuwa wamekwenda kumuona Mkuu wa Mkoa wa Iringa, waliishia katika ofisi ya Msaidizi wa Mkuu huyo wa Mkoa, Bahati Goliama.

Kwa sasa nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa inakaimiwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Asseri Msangi, ambaye wakati wanafunzi hao wakiingia ofisini kwake hakuwapo.

MGOMO WA MUCE WAENDELEA

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Elimu Mkwawa (MUCE) umeingia siku ya pili, ambapo jana wanachuo wa mwaka wa kwanza na wa pili waligoma kuingia madarasani wakishinikiza madai yao kutekelezwa na serikali.

Wanafunzi hao walianza mgomo usio na ukomo jana asubuhi hadi hapo serikali itakaporidhia madai yao ya nyongeza ya fedha za chakula na malazi kupanda kutoka Sh. 5,000 hadi 10,000.

Imeandeikwa na Romana Mallya na Eliwinjuka Shani, Dar es Salaam; Godfrey Mushi na Mawazo Malembeka, Iringa; na Emmanuel Lengwa Mbeya.



0 comments:

Post a Comment

 
BONYA HAPA