TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU / ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT CHEAP RATES | CONTACT ME: kilinyepesi@gmail.com

 photo DTB_zps7bd2662d.jpg

 photo fl_zps09337f7a.jpg


Habari Mpya:
Wednesday, January 27, 2010

Naibu Gavana Benki Kuu amtetea Liyumba

2:23 PM

Tausi Ally

NAIBU Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Juma Reli, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mpaka sasa haijajulikani kama benki hiyo imepata hasara katika utekelezaji wa mradi wa majengo yake pacha, kwa kuwa ripoti ya mwisho kuhusu mradi huo haijaandaliwa.

Reli alisema hayo jana mahakamani hapo alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi ya kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh 221 bilioni inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala wa benki hiyo, Amatus Liyumba.

Reli alisema hayo mbele ya jopo la mahakimu watatu lililokuwa lilongozwa na Hakimu Edson Mkasimongwa, baada ya kuulizwa swali na wakili anayemtetea Liyumba, Majura Magafu.

Magafu alimtaka naibu gavana huyo kuieleza mahakama kama BoT kuna hasara yoyote yoyote iliyotokana na maradi huo wa majengo pacha.

Shahidi huyo wa nane wa upande wa mashtaka alidai kuwa hadi sasa haijulikani kama kuna hasara kwa sababu ripoti ya mwisho kuhusu gharama za mradi huo haijaandaliwa.

Baada ya shahidi huo kutoa jibu hilo, Hakimu Mkasimongwa alimwambia shahidi huyo kwamba, mshtakiwa anashtakiwa kwa kosa la kuisababisha serikali hasara ya Sh221bilioni na kuwa sasa wanaitafuta hasara hiyo ilipo.

Akimjibu hakimu huyo, Reli alidai mahakama ni taasisi nzito na kubwa hivyo, hawezi kusema kitu ambacho hana uhakika nacho na baadaye akaonekana amedanganya.

Hakimu Mkasimongwa aliuuliza upande wa mashtaka endapo kesi hiyo imefunguliwa wakati usio mwafaka na kama ni hivyo; akataka umweleze kama kuna shahidi mwingine anayeweza kuthibitisha hasara hiyo kabla ripoti hiyo ya mwisho ya mradi huo haijaandaliwa.

Hakimu huyo pia ameutaka upande wa mashtaka uieleze mahakama msingi hasa wa shtaka la hasara ya Sh 221bilioni iliyopatikana katika mradi huo, wakati ripoti haijakamilika.

Awali katika majibizano yake na Wakili Magafu, Reli aliieleza mahakama kuwa aliteuliwa na rais kushika nafasi hiyo Februari 2005 na kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mkurugenzi wa Chuo cha Fedha Zanzibar.

Alisema moja ya majukumu yake kama naibu gavana ni kuingia katika vikao vya bodi ya wakurugenzi kama naibu Mkurugenzi wa bodi ya wakurugenzi ya BoT, kufanya kazi za kila siku za benki na kuingia katika vikao vya bodi.

Aliendelea kueleza kuwa katika benki hiyo kuna matumizi ya aina mbili; yakiwemo ya ya kawaida na ya kuendelea ambayo yote ili yaweze kufanyika lazima, idara husika iwajibike kupeleka mapendekezo kwa bodi ili kupata ruhusa.

Baada ya maelezo hayo, Wakili Magafu alimhoji shahidi huyo: "Nani alikuwa na maamuzi ya mwisho ya nini kifanyike na nini kisifanyike?”

Shahidi: Reli.

Wakili: Kwa mujibu wa taratibu kuhusu mradi huo, nani alikuwa na maamuzi ya mwisho kwa mradi wa majengo pacha?

Shahidi: Ni bodi ya Wakurugenzi.

Wakili: Katika kipindi chote ulichokaa BoT, mkurugenzi wa idara yoyote anaweza kufanya maamuzi bila ya gavana kujua na yakafanyiwa kazi na yakapitishwa na bodi ya wakurugenzi?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Wakati mradi unaendelea mkurugenzi wa utumishi na utawala aliwahi kuiandika mapendekezo au ombi linaloenda tofauti na matakwa ya menejimenti au gavana?

Shahidi: Mimi sikumbuki.

Wakili: Ni watu gani wengine tofauti na Liyumba waliokuwa wanahusika kusimamia au kuendesha mradi huo?

Shahidi: Meneja wa Mradi, Deogratius Kweka.

Wakili: Kuna wakati wowote mkurugenzi wa fedha aliwahi kulalamikia matumizi mabaya ya fedha katika mradi huu?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Utakubaliana na mimi kuwa mkurugenzi wa utumishi alifanya shughuli zake kwa maelekezo ya kikazi?

Shahidi: Kwa yale ninayoyafahamu mimi.

Januari 27,2008, Liyumba na Deograthias Kweka ambaye alikwiachiwa, walifikishwa katika mahakama hiyo wakikabiliwa na tuhuma hizo.

Awali katika kesi hiyo, Wakili wa Serikali, John Rwabuhanga alidai mbele ya Hakimu Mkazi Hadija Msongo kuwa kati ya mwaka 2001 na 2006, Liyumba akiwa mwajiriwa wa serikali, alitumia vibaya madaraka yake kuidhinisha malipo ya ujenzi wa minara pacha bila idhini ya bodi ya wakurugenzi wa BOT na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh221, 197, 229, 200.95 bilioni.


0 comments:

Post a Comment

 
BONYA HAPA