BAADHI ya wananchi wa jimbo la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro wamesema, hawadanganyiki na utitiri wa wanasiasa wanaojitokeza hivi sasa kwa lengo la kupambana na mbunge wao, Dk. Cyril Chami (CCM).
Wakizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wanaotembelea jimbo hilo jana, wananchi hao walisema hivi karibuni kwamba kumeibuka kundi la wanasiasa wanaobeza maendeleo yaliyofanywa na mbunge wao, jambo ambalo wanasema hawakubaliani nalo kamwe.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Kariwa, Michael Masawe, alisema maendelo makubwa yaliyofikiwa katika jimbo hayawezi kuwafanya wananchi hao kukubali kubadilishwa mawazo na kundi la watu wachache.
“Katika siku za karibuni kumekuwa na wanasiasa wanaotembelea jimbo hili na kusema mbunge aliyepo hajafanya kitu… nawaambia kwamba sisi hatudanganyiki kwa muda huu labda atafute sehemu nyingine na si wakati huu,” alisemea Masawe.
Alisema kutokana na hali hiyo, maendeleo yaliyofikiwa ndani ya jimbo hilo yanatia moyo tofauti na wabunge wote waliotangulia.
Aliongeza kuwa juhudi kubwa zinazofanywa na Dk. Chami kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zimefanikiwa kujenga shule 42 katika kata 16 za jimbo ambazo kwa kipindi kirefu watoto jimboni hapo walikuwa wakikosa nafasi za kujiunga na elimu ya sekondari.
Naye Diwani wa Kata ya Uru Kusini (Mawera), Stephen Mamboleo, alisema tangu Dk. Chami alipochaguliwa, amefanikiwa kuweka mtandao wa barabara ambazo zinapitika jimbo zima tofauti na watanguzi wake.
Alisema mbali ya hilo, amefanikiwa kusambaza vitabu kwa shule za sekondari na msingi vinavyokadiriwa kufikia thamani ya sh milioni 400 kitendo kilichosaidia kuondoa kero iliyokuwepo kwa kipindi kirefu.
Diwani huyo alisema hivi karibuni mbunge huyo amehamasisha ujenzi wa bweni katika shule ya wasichana ya Mawera kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi Kilimanjaro (KINAPA) kwa gharama ya sh milioni 130.
0 comments:
Post a Comment