TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU / ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT CHEAP RATES | CONTACT ME: kilinyepesi@gmail.com

 photo DTB_zps7bd2662d.jpg

 photo fl_zps09337f7a.jpg


Habari Mpya:
Wednesday, August 12, 2009

Mengi: Mikakati ya kudhibiti VVU, iwe pacha na ya kupambana na malaria

1:55 PM

Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Limited, Reginald Mengi, ameshauri kuhusisha udhibiti wa malaria katika mikakati ya kupiga vita maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), ili kufanikisha Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) ifikapo mwaka 2015.

Lengo namba sita la MDGs linazungumzia kupunguza maambukizi ya VVU, kifua kikuu, malaria na magonjwa mengine.

Mengi alisema hayo jana wakati akifungua mkutano wa kujadili VVU na ukimwi, na maonyesho yaliyoandaliwa na Chama cha Wafamasia nchini (PST) jijini Dar es Salaam.

“Nimetaja lengo namba sita la MDGs ili ikiwezekana mhusishe masuala ya malaria katika mkakati wa VVU na ukimwi, haya ni magonjwa 'pacha' ambayo yanaiathiri jamii yetu,” alisema.

Mengi alisema umuhimu wa kudhibiti malaria unatokana na sababu mbalimbali, zikiwemo kuwa ugonjwa unaoongoza kwa kusababisha vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na kuchangia mtu anayeishi na VVU kuugua ukimwi.

Pia, Mengi aliwataka wafamasia kuchagua dawa bora zenye gharama nafuu, ili kuwawezesha wananchi wengi kumudu kuzinunua.

Mengi alitoa wito kwa wafamasia kuishawishi serikali, iboreshe kanuni zinazotoa mwanya kwa watu wasiokuwa na taaluma hiyo (ufamasia), kuuza dawa kwenye maduka binafsi ya dawa za binadamu.

Kwa upande wake, Rais wa PST, Dk. Ambros Haule, alisema mjadala kuhusu VVU na ukimwi umepewa kipaumbele katika mkutano huo kutokana na athari zake kisiasa, kiuchumi na kijamii.

“Pamoja na jitihada zinazofanyika, watu wanazidi kuathirika kutokana na VVU na ukimwi, uchumi unaporomoka na tunarudi nyuma kimaendeleo,” alisema.

Dk. Haule, alisema kutokana na hali hiyo, wafamasia watazijadili hoja hizo ili kuainisha wajibu wa sekta hiyo katika mapambano dhidi ya VVU, Ukimwi, kifua kikuu, malaria na magonjwa mengine.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Famasia, Zarina Madabida, alisema ongezeko la watu lisilowiana na idadi ya wafamasia, ni miongoni mwa vyanzo vya kushamiri kwa wasiokuwa wataaluma kutoa huduma za ufamasia.

Madabida, alitoa rai kwa sekta binafsi kusaidia jitihada za serikali zinazolenga kuongeza idadi ya wafamasia, kwa kufungua shule na vyuo vya ufamasia.


0 comments:

Post a Comment

 
BONYA HAPA