
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Anthony Mayala (69), amefariki dunia ghafla katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Taarifa za kifo cha Askofu huyo zilithibitishwa jana na Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Method Kilaini, alipozungumza na gazeti hili.
Askofu Kilaini alisema alipata taarifa za kuugua kwa Askofu Mayala jana asubuhi.
Alisema baada ya muda mfupi, alipata taarifa kwamba hali yake ni mbaya na kwamba Kanisa lilikuwa likifanya utaratibu wa kumpeleka Nairobi kwa matibabu zaidi.
Askofu Kilaini alisema marehemu Askofu Mayala aliweza kulitumikia Kanisa kwa miaka 39 tangu 1970 alipopata daraja la Upadre.
Alisema Aprili, 1979 aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Musoma na Februari 1980 alihamishiwa Mwanza ambako alikuwa Askofu Mkuu hadi mauti yalipomkuta.
Alisema Askofu Mayala alizaliwa Aprili 23, 1940, Mwabagole, Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza.
Aliongeza mipango ya mazishi inafanywa na Mapadre na Maaskofu walio karibu na Mwanza.
Habari zaidi zilizopatikana kutoka kwa mwandishi wetu wa Mwanza, Grace Chilongola zilisema kuwa marehemu Askofu Mayala aliamka jana asubuhi akilalamika kuwa anajisikia vibaya na moyo unamuuma.
Makamu wa Askofu wa Jimbo hilo, Padre Renatus Nkwambe alisema baada ya kupata taarifa hizo, walimpeleka hospitali ya Bugando lakini baadaye mchana alifariki dunia.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Bugando, Dk. Josephat Maginga, alisema Askofu Mayala alifariki dunia kutokana na ugonjwa wa moyo.
0 comments:
Post a Comment