Eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam linakabiliwa na mrundikano wa uchafu baada ya makampuni ya kuzoa takataka kugoma kufanya kazi hiyo.
Nipashe jana ilishuhudia uchafu ukiwa umewekwa kwenye mifuko midogo midogo ya nailoni na kutupwa barabarani katika mitaa mbalimbali eneo la Kariakoo.
Baadhi ya mitaa hiyo ni ile ya Kongo, barabara za jirani na soko la Kariakoo, Swahili na Narung'ombe.
Wafanyabiashara wenye maduka katika eneo hilo, waliliambia Nipashe kuwa hali hiyo imezidi kuwa mbaya kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Selemani Musa alisema kabla ya mgomo huo magari yalikuwa yakipita asubuhi na kukusanya uchafu unaokuwa umewekwa pembeni mwa barabara lakini kwa sasa kazi hiyo haifanyiki.
Alisema kwa sasa haoni magari yakipita licha ya kuwa bado anaendelea kulipa fedha kwa ajili ya kupatiwa huduma hiyo ya kuzoa takataka.
Mwananchi mwingine, Haji Makame alisema uchafu uliowekwa pembeni mwa barabara unawapa usumbufu watu wanaopita kwa miguu.
Alisema kwa sasa analipa fedha mara mbili kwa Manispaa pamoja na kuwalipa watu wa kawaida ili wazoe uchafu unaokuwa umewekwa mbele ya duka lake.
Aliongeza kuwa kila asiku asubuhi anakuta uchafu umewekwa mbele ya sehemu yake ya biashara na kwamba analazimika kuuzoa ili kuwapa nafasi wateja wake kufika dukani kwake.
Akizungumza na Nipashe, Ofisa uhusiano wa Manispaa ya Ilala, Lucy Semindu alikataa kusema wanachukua hatua gani za dharura ili kuondoa hali hiyo.
Alisema kesi ipo mahakamani na hivyo hawezi kuzungumzia suala hilo mpaka hapo uamuzi utakapotolewa.
"Siwezi kusema lolote wakati kuna kesi mahakamani labda usubiri mpaka uamuzi utolewe" alisema.
Alipoulizwa mahakamani kuna kesi kuhusu kitu gani pia alikataa na kusema kuwa hana jibu.
Hata hivyo, alikiri kuwa Kariakoo kuna hali mbaya na kwamba Manispaa haiwezi kufanya chochote mpaka hapo uamuzi wa mahakama utakapotolewa.
Baadhi ya wananchi katika eneo hilo la Kariakoo waliozungumza na Nipashe walidai kuna mgogoro kati ya makampuni ya kuzoa takataka na Manspaa ya Ilala lakini wakasema hawajui unahusu kitu gani.
Maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam hasa katika masoko yanaongoza kwa uchafu licha ya kuwa wafanyabiashara katika sehemu hizo wanalipa ushuru wa kuzoa takataka.
1 comments:
Sasa kipindupindu kikilipuka, si itakuwa balaa
Post a Comment