RAIS Jakaya Kikwete, amekitaka Chama cha Madakatari Wanawake Tanzania(Mewata), kuanza kuwatibu wanawake wenye saratani ya uzazi, ili waweze kufikia malengo ya milenia ifikapo 2015.
Rais Kikwete alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akifungua kongamano la Jumuiya ya Kimataifa la Madaktari Wanawake lilioandaliwa na Mewata.
Alisema serikali iko tayari kusaidia fedha kwa madaktari hao kama zitahitajika na kwa hiyo, wajitahidi kutoa huduma hadi katika maeneo ya vijijini, ili kuwaokoa wanawake.
"Serikali yangu iko pamoja na nyie na iko tayari kuwasaidia. Ninafurahia hatua mliyofikia katika kupambana na saratani ya matiti kwa wanawake," alisema Rais Kikwete.
Alisema serikali ilikuwa tayari kuwasaidia wanawake na ndiyo maana imeongeza fedha katika bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, katika mwaka wa fedha wa 2009/10.
``Chama kama Mewata wana kazi muhimu ya kufanya katika kuboresha afya za wanawake na vile vile kupunguza vifo vya wajawazito,`` alisisitiza rais.
Kwa mujibu wa maelezo yake kwa sasa idadi ya wanawake wanaokufa katika hatua za kujifungua ni 578 katika kila kundi la wanawake 1,000 wanaojifungua kila mwaka.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa, alisema Tanzania bado haijafanya vizuri katika kufanikisha malengo ya milenia hasa katika kupunguza vifo vya wajawazito.
Aliwataka wanawake kote nchini, kuhudhuria mara kwa mara matibabu ya saratani ya uzazi, pale wanapohisi mabadiliko ambayo si ya kawaida.
``Wanawake lazima wajue hali zao kiafya, kwa hiyo wawe wanakwenda mara kwa mara kupata huduma, hiyo ndiyo njia rahisi ya kupambana na saratani ya uzazi ambayo inawatesa,``alisema Profesa Mwakyusa.
Mwenyekiti wa Mewata, Dk Marina Njelekela, alisema malengo ya milenia yanashindwa kufikiwa kutokana na matatizo ya njaa, utapiamlo na umasikini.
Hali kadhalija matatizo ya kisiasa na mgogoro wa uchumi unaondelea duniani hivi sasa.
0 comments:
Post a Comment