Kituo cha Redio Maria cha Kanisa Katoliki nchini, leo kinaanza kukusanya michango kupitia huduma ya Vodafone M-Pesa ambapo fedha zitakazopatikana zitatumika kueneza huduma za kituo hicho nchini.
Akizungumzia suala hilo jana Dar es Salaam, Mratibu wa redio hiyo, Johanna Hulatsch, alisema wasikilizaji wa kituo hicho wataweza kutuma michango yao na kujifunza kupitia matangazo ya moja kwa moja yanayorushwa na redio hiyo.
“Tunatarajia michango ya wasikilizaji wetu kwa sababu redio yetu sio ya kibiashara kama zilivyo zingine. Watu wanakipenda kituo chetu kwa sababu inasaidia kubadilisha maisha yao nao ndio wanaoguswa katika kuisaidia redio yetu," alisema Hulatsch. Alisema kwa kutumia huduma ya Vodafone M-Pesa watu wataweza kutuma hata kiwango kidogo cha fedha kutoka katika maeneo hata yaliyoko pembezoni mwa miji, wilaya, kata na hata vijiji.
Mbali na hayo, redio hiyo ya Kanisa Katoliki pia inarusha vipindi mbalimbali vinavyowapa nafasi waumini kusali, kujifunza kukomunika na kuelimisha ushajihishaji wa masuala mbalimbali ya kijamii. Hadi sasa, Redio Maria imerusha matangazo yake karibia kila mahali, kwa kuwanasa wasikilizaji katika masuala yanayowagusa na yaliyokuwa yakiwakosesha imani na malengo yao mbalimbali.
Kwa mujibu wa Hulattsch, kituo hicho kimebadilisha maisha ya jamii kubwa kupitia katika vipindi vyao mbalimbali vinavyolenga katika kilimo, masuala ya afya bora yanayozikabili familia nyingi hususani za vijijini. Kituo hicho cha redio kilianza rasmi kurusha matangazo yake nchini Aprili 1996, mjini Songea ambapo kwa sasa kinapatikana takribani maeneo yote nchini kupitia satelaiti.
0 comments:
Post a Comment