Kenya imesema mtu wa kwanza amegundulika nchini humo akiugua ugonjwa wa homa ya mafua ya nguruwe unaotokana na vurusi vya H1N1.
Waziri wa Afya ya Jamii, Beth Mugo, aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba mgonjwa huyo wa kwanza wa ugonjwa huo hatari ni kijana wa miaka 20 anayesoma nchini Ungereza. Hakumtaja jina.
"Hii ni mara ya kwanza kugundua mtu mwenye mafua ya nguruwe hapa Kenya," alisema waziri huyo. Alisema kundi la wanafunzi 30 waliongia nchini humo hivi karibuni wamezuiliwa katika hoteli moja katika jiji la Kisumu, magharibi mwa Kenya wakichunguzwa.
Hata hivyo, Mugo alisema mwanafunzi aliyethibitika kuwa na H1N1 anaendelea na matibabu na kwamba Wakenya hawapaswi kuwa na mashaka kwa sababu serikali imejiandaa kwa matibabu.
Juzi, gazeti la Standard la Kenya lilimkariri Waziri Mugo liliandika kwamba baada ya mwanafunzi huyo aliyewasili Kenya toka Juni 20 kupelekwa katika hospitali moja ya serikali akiwa hoi, madaktari na wauguzi walionekana kumkimbia kumtibu, kwa hofu ya wao pia kuambukizwa, hatua iliyoifanya serikali kuingilia kati.
Gazeti hilo lilimkariri juzi Waziri Mugo akitoa onyo kwa maofisa wa afya kuheshimu taaluma zao na kutibu wagonjwa bila uoga.
Wanawake wawili wa Ivory Coast ambao walirejea hivi karibuni kutoka Brussels, Ubelgiji, waligundulika juzi kwamba nao wanaumwa mafua ya guruwe ambapo Shirika la Afya Duniani (WHO) lilithibitisha kwamba wanachoumwa ni mafua ya nguruwe.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza, Reuters, nchi nyingine za Afrika ambazo hadi jana zimethibitika kuwa na wagonjwa wa mafua ya nguruwe ni Afrika Kusini na Ethiopia. Ugonjwa wa mafua ya nguruwe umeshawapata watu zaidi ya 67,000 katika nchi 113 na tayari umeshaua watu 263 duniani kote, kwa mujibu wa taarifa za WHO.
Dalili za mafua ya nguruwe ni pamoja na homa kali, kukohoa, kuvimba koo, mwili kuuma, kichwa na mwili kuwa mchovu.Wakati huohuo, serikali ya Tanzania imesema imeshanza kuchukua hatua kudhibiti ugonjwa huo.Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa, alikiri kupata taarifa hiyo, kupitia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) katika matangazo yake yaliyosikika jana jioni.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana kutoka mjini Dodoma, Profesa Mwakyusa alisema kutokana na taarifa hiyo, amewaagiza wataalamu wa afya waliopo mipakani hususani katika mpaka wa Tanzania na Kenya, Namanga na viwanja vya ndege, kuongeza umakini katika kuwabaini na kuwapima wageni wanaoingia nchini wenye kutia shaka.
Hata hivyo, Profesa Mwakyusa, alisema kugundulika kwa mgonjwa huyo, hakutatoa fursa ya kuwapima wageni wote watakaoingia nchini kutokea Kenya. “Kwa mujibu wa maelekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO), kumchunguza kila anayeingia itakuwa ni sawa na kuwanyanyapaa,” alisema.
Pia alisema jitihada zinafanywa kwa kuwasiliana na waongozaji wa vyombo vya usafiri, hasa marubaini ili kupata taarifa ikiwa watakuwa na abiria yeyote anayeshukiwa kuwa na ugonjwa huo, ili apimwe mara anapowasili nchini.
0 comments:
Post a Comment