TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU / ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT CHEAP RATES | CONTACT ME: kilinyepesi@gmail.com

 photo DTB_zps7bd2662d.jpg

 photo fl_zps09337f7a.jpg


Habari Mpya:
Tuesday, December 15, 2009

Watakaopandisha nauli kulimwa faini 200,000/-

7:07 PM

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini nchini (Sumatra), imetoa ufafanuzi kuhusu adhabu itakayowakumba wamiliki wa mabasi ya mikoani watakaofanya makosa ya kupandisha nauli kiholela, kwa kusema kwamba, yatatozwa faini ya Sh. 200,000.

Meneja wa Mawasiliano wa Sumatra, David Mziray, alisema jana kuwa wanaendelea na mikakati ya kujiimarisha kutekeleza kampeni ya kuwadhibiti wanaotenda makosa hayo.

“Kwa jumla, makosa yote ya nauli adhabu yake ni faini ya sh. 200,000 na si sh. 100,000 kama ilivyoripotiwa jana,” alisema Mziray.

Sumatra imetoa onyo hilo zikiwa zimesalia wiki mbili kuingia vipindi vya Sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya, ambavyo baadhi ya wamiliki na mawakala wa kampuni za mabasi hayo, huvitumia kupandisha nauli kwa abiria pamoja na mizigo.

Juzi, Mziray alikaririwa akisema kwamba, kampeni ya kudhibiti mabasi hayo dhidi ya vitendo hivyo, inatarajiwa kuanza kufanywa na Mamlaka hiyo wiki hii nchini kote.

“Napenda kutumia nafasi hii kuwaonya wamiliki wa mabasi watakaojaribu kupandisha nauli kinyume na ile inayotambuliwa na Sumatra kwamba, watachukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kutozwa faini. Na abiria watarejeshewa kiasi cha fedha kilichozidi katika nauli halali,” alisema Mziray.

Aliongeza kuwa wamekuwa makini dhidi ya watu wanaopandisha nauli za mabasi kiholela na kwamba, walianza kujipanga kudhibiti kero hiyo miaka miwili iliyopita, kwa vile imekuwa ikifanywa kwa nia mbaya ya kuwakomoa wananchi.

Alisema mkakati huo umekuwa ukitekelezwa na Sumatra katika vituo mbalimbali vya mabasi, ambavyo vimekuwa sugu katika kutumiwa na wajanja hao kuendesha vitendo hivyo, kikiwamo Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo (UBT), jijini Dar es Salaam na cha Kibaha, mkoani Pwani.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka abiria kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha wanajiorodhesha mapema kwenye kitabu cha abiria (booking) na kukata tiketi kwenye ofisi za kampuni za mabasi ili kuepuka kulanguliwa tiketi na wajanja wachache walioweka mawindo yao kwenye vituo hivyo.


0 comments:

Post a Comment

 
BONYA HAPA