TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU / ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT CHEAP RATES | CONTACT ME: kilinyepesi@gmail.com

 photo DTB_zps7bd2662d.jpg

 photo fl_zps09337f7a.jpg


Habari Mpya:
Sunday, December 20, 2009

'Inasikitisha''Ajali ya Mohamed Trans: Simulizi za mikosi ya familia za zizimisha

8:48 PM

SIMANZI, vilio na majonzi jana vilitawala katika Kijiji cha Mamba Kotela wakati wa mazishi ya ndugu sita wa familia moja ya Maleko waliofariki juzi wakienda katika harusi ya Egbert Maleko iliyokuwa ikitarajiwa kufanyika leo.

Ndugu hao Geofrey Maleko (70) mkazi wa Mbezi, James Maleko (32) na mtoto wake Mary James (6), Teoflas Maleko (42) na mkewe Grace Maleko (42) ambao ni wakazi wa Tabata Kisukuru pamoja na baba mdogo wa bwana harusi, Martin Maleko (68) mkazi wa Tabata na Johnson Moshi (14).


Ndugu hao walizikwa katika eneo moja la shamba la familia ya Maleko ambapo kijana Johnson Moshi alizikwa pembeni kidogo na eneo walilozikwa wenzake kwa maelezo yaliyotolewa na familia hiyo kuwa ni mtoto wa upande wa wajomba.


Akizungumza kwa niaba ya ukoo wa Maleko, Rumisha Maleko aliwaomba viongozi wa dini na serikali kuwa karibu na kijana wao ambaye alitarajiwa kufunga ndoa iliyotarajiwa kwenda sanjari na sherehe za kipaimara za watoto wao.


Alisema kijana huyo ana wakati mgumu kwa sasa kwani mwaka jana alipatwa na matatizo baada ya kuvamiwa na majambazi katika duka lake ambapo alifanikiwa kuwaua kwa kuwapiga risasi.


Hata hivyo wiki moja baada ya tukio la kuua majambazi hao, wakati mke wa kijana huyo akiwa nyumbani kwake, alisikia mlio wa bomba la gari la kutolea moshi uliomshtua na kufariki dunia papo hapo kwani alifikiri ni majambazi wamekuja tena kumdhuru.


Kutokana na tukio hilo kijana huyo aliamua kumtafuta binti mwingine kwa ajili ya kufunga ndoa ambapo wakati wakiwa katika hatua za mwisho ndipo ikatokea ajali hiyo na kuwapoteza ndugu zake saba huku wengine wakiwa katika hali mbaya katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.



Akizungumza katika ibada ya Mazishi iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisis ya Kaskazini Usharika wa Kimangaro Mamba, Askofu wa Dayosisi hiyo, Dk. Martin Shao alisema kuwa msiba huo haujagusa kanisa tu wala familia bali umegusa Taifa zima.


Alisema kuwa pamekuwepo ajali nyingi za mara kwa mara ambazo hupoteza maisha ya watu wasio na hatia kutokana na kukosekana kwa hekima na uzembe na wala si kwa mipango ya Mungu.


"Ajali nyingi zinatokana na uzembe wa watu wanaopenda kuharakisha mambo, madereva wetu wangekuwa makini na waangalifu na wakatembea kwa mwendo unaokubalika, ajali hizi zisingejitokeza na wala tusingepoteza maisha ya watu wengi kwa ajali za mara kwa mara," alisema.


Aidha alisema vifo vingi husababishwa na watu wasio na hekima wenye kutumia dawa za kulevya na nguvu za giza lakini kama yakipunguzwa mambo hayo, pakawepo hekima ambayo itaokoka roho za watu wengi.


Alisema Mkoa wa Kilimanjaro utafanya maombi Januari 2010 yatakayowashirikisha wachungaji na watumishi kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuombea Taifa na Bara la Afrika kwa ujumla ili kuondoa maovu na kurejesha hekima iliyopotea.


Kwa upande wake mchungaji aliyekuwa akiongoza ibada ya mazishi, Rodrick Mlay aliwataka wafiwa kuwa na roho za subira wakimuomba Mungu na kuitaka serikali kuichunguza kamapuni ya Mohamed Tras ambayo basi lake ndiyo chanzo cha ajali hiyo.


“Yamesemwa mengi kuhusu ajali hii maana kampuni hii haina historia nzuri, haiwezekani kampuni moja ikamaliza watu wengi kiasi hicho, maana ni zaidi ya ajali tatu zimeshatokea na kuhusisha kampuni ya Mohamed Trans huku watu zaidi ya 100 wakipoteza maisha… kwa kweli tunapaswa kumuomba Mungu sana kwa hili,” alisema.


Akitoa salamu za Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Monica Mbega aliwataka wafiwa kutulia na kumuomba Mungu hasa katika kipindi hiki cha majonzi huku serikali ikiendelea kuchukua hatua zaidi kutokana na tukio hilo.


Mazishi hayo yalihudhuria viongozi mbalimbali wa vyama, serikali na dini akiwemo, Mbunge wa Vunjo Aloyce Kimaro, Mbunge wa Viti Maalum mkoani Kilimanjaro, Shally Raymond, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Vicky Nsilo Swai, na Kamanda wa Polisi mkoani humo, Lucas Nghoboko.



Naye Lucy Lyatuu anaripoti kuwa jirani wa familia hiyo aliyepo Tabata Kisukuru Dar es Salaam, Baraka Elias alisema walipata tarifa za msiba huo juzi majira ya saa 12:30 jioni.


Alisema wanandugu wengine waliokuwa wamebaki Dar es Salaam walipigiwa simu na kupewa ujumbe kuhusu ajali hiyo kwa kuwa muda wote wa safari walikuwa wakipeana taarifa za kilichokuwa kikiendelea katika msafara huo.


Elias alisema safari ya wanandugu hao ilipangwa kufanyika Jumatatu Desemba 14, 2009, lakini kutokana na kuhitajika kuendelea kukusanya michango zaidi ya harusi na marekebisho madogo ya gari walilosafiria ilibidi kuahirisha safari na kusogeza mbele hadi juzi.


Hata hivyo, Elias alisema katika harusi waliyokuwa wakihudhuria bwana harusi mtarajiwa Egbert Maleko alikuwa akifunga harusi hiyo kutokana na aliyekuwa mke wake wa awali kufariki, hivyo kuruhusiwa kuoa mke mwingine.


“Wanandugu wote waliobaki Dar es Salaam wameondoka juzi saa 3:00 usiku mara baada ya kupatiwa taarifa ya msiba ili kuwahi maziko ambayo yanatarajiwa kufanyika leo (jana).


“Hapa kwa Toeflas tumebaki vijana wawili wa kazi kwa ajili ya kulinda usalama wa makazi haya,” alisema Baraka ambaye ndiye aliyebaki katika nyumba Toeflas Maleko.



1 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Bado naomba kuwa siku moja ajali hizi ziwe simulizi. atu wanaumizwa saana na wanateseka kwa miaka mingi ijayo. Ni juzi tu nimekumbuka miaka 10 ya ajali ambayo bado naendelea kupata maumivu yake.
Sijui ni hatua zipi za makusudi zifanywazo kuepusha vifo na maumivu kwa wengine wengi?
Mungu awalinde ndugu hawa na natumai watapata nguvu za kuwawezesha kuyapita haya

Na kwako Kaka Amani,
Kwa niaba ya familia yangu na wapenda mema wote nakutakia kila lililo jema wakati huu wa sikukuu na usalama kuelekea mwaka mpya
Baraka kwako

Post a Comment

 
BONYA HAPA