Washitakiwa wengine mauaji ya albino wasubiri hukumu
Kesi nyingine ya mauaji ya albino yaliyofanyika mwaka jana mkoani Shinyanga, inatarajiwa kuhukumiwa wakati wowote baada ya mahakama hiyo maalum kukamilisha usikilizaji wa mashahidi wa pande zote na kupata maoni ya wazee wa mahakama hiyo jana ambao wametaka washitakiwa wafungwe.
Tarahe ya hukumu hiyo inatarajiwa kutangazwa na Msajili wa wilaya Mahakama kuu, kanda ya Tabora.
Washitakiwa katika kesi hiyo ya mauaji ya kukusudia ya albino Lyaku Willy (51) yaliyotokea Desemba 4, mwaka 2008 katika kijiji cha Nkindwabiye wilayani Bariadi ni Mboje Mawe (49), Ncheyeye Kishiwa (65), Sayi Gamaya (48) na Sayi Mafizi (33), wote wakazi wa kijiji hicho cha Nkindwabiye.
Hukumu hiyo itakuwa ni ya pili kutolewa hapa mkoani Shinyanga baada ya ile iliyotolewa Kahama Septemba 23 mwaka huu ambapo jaji Gabriel Rwakibalila aliwatia hatiani Masumbuko Madata wa Ituga, Emmanuel Masangwa wa Bunyihuna na Chareles Kalamuji au Charles Masangwa wa Nanda, wilayani Bukombe. Watatu hao ambao wamekata rufaa wanadaiwa kumuua albino Matatizo Dunia (14) wa kijiji cha Bunyihuna, Bukombe.
Mapema jana, Jaji Mmjemas katika mahakama yake inayokaa mjini Shinyanga, alisikiliza na kupokea maoni ya wazee watatu wa mahakama hiyo yatakayomsaidia katika kutoa hukumu yake.
Katika kesi hiyo namba 25 ya mwaka 2009, wazee wa mahakama hiyo kwa kauli moja wameuponda ushahidi uliotolewa na upande wa utetezi na kusema washitakiwa wote wanne wana hatia ya kosa la mauaji ya kukusudia.
Wazee hao, Charles Luhende, Mary Wamba na Anna Ndimila walisema kuwa ushahidi uliotolewa na mtaalam kutoka ofisi ya mkemia mkuu wa serikali, Gloriah Machuve ulikuwa umesheheni utalaam wa kina huku ukibainisha wazi jinsi washitakiwa walivyohusika katika mauaji hayo kutokana na vinasaba kupatikana katika panga na kisu chao.
0 comments:
Post a Comment