WAKATI wakazi wa Mbagala wakiendelea kulipwa fidia zao, ripoti maalumu inayoweza kumuondoa madarakani Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga taifa Dk Hussein Mwinyi imewasilishwa kwake.
Ripoti hiyo ya tume iliyochunguza sababu za milipuko na mambo mengine ya kitalaamu, iliwasilishwa kwake wiki hii na kwamba kwa sasa inafanyiwa kazi ili kujua ukweli wa milipuko ya mabomu ya Mbagala.
Dk Mwinyi aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba kama ripoti ya tume itabainisha kwamba kulipuka kwa mabomu hayo kulitokea kwa uzembe wa wataalamu wake na serikali, atatekeleza ahadi yake ya kujiuzulu kwa manufaa ya umma kama alivyoahidi.
Akijibu maswali mbalimbali ya waandishi jana, Dk Mwinyi alisema ripoti ya tume iliyoundwa chini ya wizara yake ilikuwa ni kwa ajili ya kutafuta chanzo cha ajali na ndiyo maana imechukua muda mrefu kukamilika kwani iliwalazimu kuifanya kiutaalamu zaidi.
"Nimeshakabidhiwa ripoti ya mabomu Mbagala, hivi sasa ipo katika ngazi ya mwisho kabla ya kutolewa kwa wananchi, ikibainika kuwa kulikuwa na uzembe basi nitatekeleza ahadi yangu ya kujiuzulu," alisema Dk Mwinyi.
Alisema hivi sasa ripoti hiyo tayari imeshafikishwa katika ngazi husika na ya mwisho kabisa kabla ya kutolewa kwa wananchi kwa lengo la kuwafahamisha chanzo cha ajali hiyo.
Alisema pamoja na mapendekezo mengi katika ripoti hiyo suala la utaratibu wa kufuatwa katika kuepusha ajali za wananchi wanaoishi kandokando ya kambi za jeshi limepewa kipambele.
Wakati huo huo Dk Mwinyi alisema kuwa wanajeshi 600 waliosalia kwa ajali ya kwenda kulinda amani Darfur wanatarajiwa kuondoka Septemba, 9 mwaka huu kuungana na wenzao 275 waliotangulia.
0 comments:
Post a Comment