MAKAMANDA wa polisi wa Mikoa ya Kikanda, wamekutana leo Jijini Mbeya, kujadili hali ya uhalifu ikiwa na kuweka mikakati itakayosaidia kuwabana askari watakaobainika kukiuka sheria na taratibu za kazi.
Mkutano huo unafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, lengo kuu likiwa ni kujadili hali ya usalama na uhalifu wa maeneo katika Mikoa ya Morogoro, Iringa, Ruvuma, Njombe na Mbeya .
Akizungumzia mikakati hiyo, Mwenyekiti wa Mkutano Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ndugu Faustine Shilogile alisema katika kikao hicho agenda kuu itakuwa ni kujadili matukio ya uhalifu wa unyang’anyi wa kutumia silaha, matukio ya ajali pamoja na kujadili nidhamu kwa watendaji wa jeshi hilo.
Amesema Wahalifu wamekuwa na tabia ya kuhama hama mara wanapofanya tukio, hawakai sehemu moja hivyo mkutano huu utasaidia kwa wajumbe kubadilishana na kupeana uzoefu wa kazi,’alisema
Aidha, amefafanua kuwa jeshi la polisi hivi sasa kupitia baadhi ya askari limekuwa likikumbwa na matukio ya ukiukwaji wa maadili kwa kukutwa na tuhuma mbalimbali za uhalifu.
Kwa upande wake, Kamanda wa polisi wa mkoa wa mbeya, Ndugu Diwani Athumani ambaye ni mwenyeji wa Mkutano huo , alisema kikao hicho kinatarajia kutoka na mikakati itakayosaidi kupunguza wimbi la uhalifu pamoja na ajali barabarani.
Amesema mara nyingi Wahalifu wamekuwa wakitumia njia nyingi kufanya uhalifu na kukimbilia mikoa ya jirani hivyo mkutano huu ambao unahudhuriwa na Makamanda pamoja na wakuu wa upelezi utasaidia kuwabaini ikiwa na kusambaratisha mtandao uliopo
Mkutano huo ni watatu baada ya mkutano wa kwanza kufanyika Mkoani Iringa na wapili ulifanyika Mkoani Morogoro na kwamba wajumbe wanatarajia kutoka na maadhimio mapya.
Na Mbeya yetu
|