![]() |
Wanasayansi wa ndani wathibitisha uwezo wake.
Mussa Juma, Samunge
Wataalamu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii pamoja na taasisi mbalimbali za afya nchini, jana walifika
Samunge kuanza mchakato wa kutafiti dawa inayotolewa na Mchungaji,
Ambilikile Mwasapila kama inatibu magonjwa sugu au la.Wataalamu hao
walifika Samunge majira ya saa sita mchana na kusababisha kusitishwa kwa
muda utoaji wa tiba ili kuwapa nafasi ya kufanya mahojiano na Mchungaji
Mwasapila, kuchukua sampuli za dawa na mti ya mugariga. Baada ya
mahiojiano, nao pia walipata kikombe cha tiba.
Wataalamu
hao ni pamoja na Profesa Charles Wambebe wa WHO Marekani, Dk Budeba
Sylvester wa Wizara ya Afya na Dk Georges Shemdowe kutoka Tume ya
Sayansi na Teknolojia.Ujumbe wa huo pia ulimjumuisha, Mkemia kutoka
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Hamis
Malebo.
Profesa
Wambebe ambaye ni raia wa Nigeria na mtaalamu bingwa mwenye uzoefu na
masuala ya tiba za asili, alisema amefika Samunge kutokana na maombi ya
Serikali ya Tanzania iliyoomba msaada wa WHO, kufanya uchunguzi wa dawa
ya Mchungaji Mwasapila.
''Tumekuja
hapa Samunge, kufuatilia tiba hii jinsi inavyotolewa na WHO kwa
kushirikiana na Serikali ya Tanzania itaendesha utafiti kwa kuhusisha
watu waliotumia dawa, Mchungaji Mwasapila na wadau wengine ili kuona
inaponyesha kiasi gani," alisema Profesa Wambebe.
Alisema
wanatarajia kuwa ndani ya miezi 12 watakuwa wametoa majibu juu ya ubora
wa dawa hiyo na katika kipindi cha miezi mitatu ijayo watatoa maendeleo
ya utafiti ambao utakuwa unafanywa.
Alisema baada ya kukamilisha utafiti, Serikali ya Tanzania ndiyo
itakayoachiwa jukumu la kutangaza dawa hiyo kama inatibu kiasi gani na
kama itahitaji kuboreshwa ili iwe katika mazingira ya kisasa ni nini
kifanyike.
Wagonjwa wa kisukari kuanza
Dk
Sylvester alisema uchunguzi huo utaanzia kwa wagonjwa wa kisukari hasa
kutokana na vipimo vyao kuwa rahisi na kufuatilia hali zao pia itakuwa
ni rahisi tofauti na magonjwa mengine.
Alisema wizara ya afya inakusudia kupeleka Samunge, maabara kubwa ya
kisasa ambayo wagonjwa watapimwa kabla ya kunywa dawa na baada ya kunywa
watafuatiliwa kitaalamu hadi hapo itakapothibitika ubora wa dawa.
"Tunaomba
wananchi wasubiri watafiti kufanya kazi kwani tayari taarifa ilitolewa
kuwa dawa hii haina madhara kwa binadamu na kazi inayofuatia sasa ni
kutazama ubora wake katika kutibu maradhi mbalimbali," alisema.
Babu atoa shukrani
Katika
hatua nyingine, Mchungaji Mwasapila jana alitoa shukrani kwa serikali
kuanzia ngazi ya Kijiji hadi wilaya kutokana ushirikiano waliompa katika
msiba wa mtoto wake, Jackson (43) ambaye alifariki wilayani Babati
baada ya kuugua malaria.
"Napenda kushukuru Serikali Wilaya ya Ngorongoro na Babati kwa msaada
mkubwa ambao wamenipa katika msiba na kuniwezesha kufika kwa wakati na
kurejea hapa, pia nawashukuru wananchi wote kwa ushirikiano walionipa,"
alisema Mwasapila.
Habari zaidi: Bofya Hapa
|
Saturday, April 30, 2011

0 comments:
Post a Comment