Tiba ya Mchungaji Mstaafu wa KKKT, Ambilikile Masapile ‘Babu’ anayotoa
huko Loliondo, Arusha inadaiwa kuingia hatua ya pili baada ya hivi
karibuni kufanya maajabu zaidi.
Kwa mujibu wa shuhuda wetu,
maajabu ya tiba hiyo yaliwakuta wanawake wawili, mmoja ambaye jina lake
halikupatikana mara moja, alitapika nyoka muda mfupi baada ya kunywa
dawa ya Babu na kuibua hisia kali miongoni mwa watu waliokuwa kwenye
foleni wakisubiri huduma.
Shuhuda huyo alisema kuwa, mwanamke
mwingine aliyejulikana kwa jina moja la Saumu, yeye alijikuta
akijifungua ‘minyama’ (kama steki ya ng’ombe) baada ya kupata kikombe
hicho cha Babu Masapile.
Alisema kuwa, awali, mwanamke
aliyetapika nyoka alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya tumbo yasiyo na
mfano ambapo ameshakwenda hospitali mbalimbali, ikiwemo kwa waganga wa
kienyeji bila mafanikio.
Aliendelea kudai kwamba, siku ya tukio,
mwanamke huyo, baada ya kunywa dawa ya Babu, saa chache baadaye alianza
kuhisi kichefuchefu kilichoambatana na kutema mate kwa wingi.
“Alianza
kusikia kichefuchefu, akawa anatema mate, mwisho ikaja hali ya
kutapika, ndipo nyoka mweupe alipotoka kinywani mwake na kuangukia
chini,” alisema shuhuda.
Alisema, baada ya tukio hilo, mwanamke
huyo alijisikia mzima wa afya na kuamini amepona tatizo la tumbo
lililomtesa miaka nenda, rudi.
Aliendelea kusimulia kuwa, kwa
upande wake, Saumu, yeye alikuwa kwenye foleni akifukuzia kikombe cha
Babu kutokana na matatizo ya kutopata ujauzito tangu ameolewa.
Alidai
kwamba, saa chache baada ya kunywa dawa ya Mchungaji Masapile, alianza
kuhisi tumbo kuvimba na kuwa kubwa mfano wa mjamzito.
Shuhuda
huyo alisema kuwa, ilifika mahali alipoeleza anavyojisikia, baadhi ya
wanawake walimwambia ni mimba jamko ambalo lilisumbua akili ya Saumu
akiamini haiwezekani apate ujauzito baada ya kupata kikombe.
Aliendelea
kudadabua kwamba, baada ya tumbo kukua zaidi, alianza kuhisi maumivu
makali ambapo alipoyasimulia, wanawake walimwambia ni dalili ya uchungu
wa kuzaa.
Alidai kuwa, kilifika kipindi kingine kwa mwanamke huyo
ambapo alisaidiwa ili ajifungue lakini cha ajabu, lilitoka pande la
nyama kama kilo moja ya steki ya ng’ombe na kuwafanya watu kubaki vinywa
wazi.
Baadhi ya watu walioshuhudia matukio hayo walisema kuwa,
sasa wanaamini dawa ya Babu inaponya hata magonjwa ya kurogwa wakidai
matukio yote mawili ya wanawake hao yametokana na nguvu za giza.
“Hawa
matatizo yao si ya kidaktari, itakuwa nguvu za giza. Naamini dawa ya
Babu inaponesha hata mtu aliyerogwa,” alisema mwanaume mmoja ambaye yuko
kwa Mchungaji huyo kwa ajili ya mkewe anayesumbuliwa na presha mara kwa
mara.
Hivi karibuni, Babu alitamka kuwa, ili mtu apone kwa
kutumia dawa yake anatakiwa kutanguliza imani ya kiroho huku
akijifagilia kwamba, tiba yake ina mkono wa Mungu kwa asilimia mia moja.
Maandiko Matakatifu ya Wakristo (Babu ni muumini wake) yanasema kwa Mungu hata nguvu za giza zinashindwa | |
0 comments:
Post a Comment