.jpg)
Serikali imekwepa kutoa majibu juu ya hatua inazotarajia kuchukua dhidi ya watu wanaotuhumiwa kupokea rushwa katika ununuzi wa rada kama ilivyopendekezwa na Uingereza.
Hivi karibuni, kampuni ya BAE iliyoiuzia Tanzania rada ilikiri kuwa kulikuwa na rushwa katika ununuzi wa rada na kukubali kulipa faini huku Uingereza ikiishauri serikali ya Tanzania kuchukua hatua inazoona zinafaa dhidi ya watu waliohusika.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambayo imepewa jukumu la kuchunguza masuala ya rushwa imesema haijui kitu chochote kuhusu sakata hilo. Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Habari wa Takukuru, Doreen Kapwani, alisema hajui kitu chochote kuhusiana na sakata hilo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, alipoulizwa jana alijibu kwa kifupi kuwa hawezi kuzungumza na magazeti kupitia kwenye simu. “Muulize ofisa habari wangu, mimi siwezi kuongea na vyombo vya habari kwenye simu,” alisema.
Baada ya kutamka maneno hayo Dk. Hosea alimkatia simu mwandishi na alipopigiwa tena ili aulizwe maswali zaidi hakupatikana tena.
Nipashe ilitaka ufafanuzi kutoka Takukuru baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, kusema kuwa kauli nzuri kuhusu sakata hilo inaweza kutolewa na taasisi hiyo kwa kuwa wao ndio wanaohusika na uchunguzi wa tuhuma za rushwa.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, alipoulizwa alisema hajui chochote kwa kuwa yuko likizo.
Hata hivyo licha ya Nipashe kumueleza sakata zima linalohusu ununuzi wa rada aliendelea na msimamo wake kuwa hajui kitu kuhusu suala hilo.
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi, alipoulizwa kuhusu sakata hilo alijibu kwa kifupi kuwa hajapelekewa jalada lolote ili aandae mashtaka.
“Mimi sijaletewa jalada lolote na mimi ofisi yangu haifanyi uchunguzi bali inapokea majalada na kuyafanyia kazi," alisema.
Wakati mamlaka za serikali zikishindwa kulitolea ufafanuzi suala hilo, Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, amesema kuwa anashangazwa na serikali kukaa kimya dhidi ya watuhumiwa.
Alisema jana kuwa serikali ingeweza kutumia taarifa ya SFO kuwashughulikia watu wanaotuhumiwa kuhusika katika kashfa hiyo.
Dk. Slaa ambaye pia ni Mbunge wa Karatu, alisema uamuzi wa BAE kukubali kulipa faini ni baada ya kuona kuwa kulikuwa na kiasi kikubwa cha fedha kilichokuwa kimezidi katika manunuzi ya rada hiyo.
Aliahidi kuwa ataendelea kupiga kelele kupitia bungeni ili serikali ichukue hatua dhidi ya watuhumiwa.
0 comments:
Post a Comment