TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU / ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT CHEAP RATES | CONTACT ME: kilinyepesi@gmail.com

 photo DTB_zps7bd2662d.jpg

 photo fl_zps09337f7a.jpg


Habari Mpya:
Wednesday, February 10, 2010

Mbeya wasubiri kwa hamu uwanja mpya wa ndege wa Songwe

1:32 PM
Ujenzi umekamilika kwa asilimia 75
Ndege za Boeing 737 zitaweza kutua

TAKRIBANI Kilometa 80 kutoka kwenye Uwanja mpya wa Ndege unaojengwa eneo la Songwe katika Wilaya ya Mbeya Vijijini, zinasikika sauti za “mia zote”… “mia zote”; ikiwa na maana ya bei ya ndizi mbivu za wingi wa vichana vitatu.

Bei ikiongezeka sana basi hufika Shilingi 1,000 kwa vichana hivyo vitatu vya ndizi mbivu aina ya kisukari au Shilingi 1,500 kwa mkungu mmoja wa ndizi hizo.

Hizo ndizo bei za ndizi unazozipata eneo la Kiwira katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya. Ni wazi ni ‘bei ya kutupwa’, lakini wananchi wale hawana namna nyingine kutokana na kukosa soko nzuri kwa bidhaa zao hizo za ndizi. Wanalazimika kuuza ili angalau wajipatie pesa kidogo kwa ajili ya kununulia mahitaji yao mengine.

Ndizi ni bidhaa zenye kuharibika. Ni mazingira hayo yanayowalazimisha wananchi wale kuuza ndizi zao kwa ‘bei ya kutupwa’ kwa wasafiri wapitao eneo hilo.

Pamoja na kupata ndizi kwa ‘bei ya kutupwa’, eneo la Kiwira au Mwankenja kama linavyofahamika kwa wenyeji, ni maarufu vile vile kwa bidhaa za matunda mbalimbali kama vile maparachichi, mapohora, na mananasi.

Bidhaa zote hizo za kilimo huuzwa kwa bei ya chini sana kiasi cha wageni wengi kutoamini pale wanapotajiwa bei zake. Hujihisi kana kwamba wanawaibia, lakini hiyo ndiyo hali halisi kwa wakulima hao wa Wilaya ya Rungwe. Hawana pa kupeleka bidhaa zao, wafanye nini.

Kiwira ni sehemu ndogo tu ya wakulima katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Ruvuma na Rukwa ambao hulazimika kuuza bidhaa zao za kilimo kutokana na kukosekana kwa soko la uhakika. Bado wategemea soko la ndani ambalo haliwapatii bei nzuri itakayowawezesha kuondokana na umasikini.

Na mazingira haya yanayowafanya wakulima wa ndizi na maparachichi mkoani Mbeya, pamoja na wale wa mazao mengine kutoka ukanda huo, kuwa na hamu kubwa ya kuona Uwanja wa Ndege wa Songwe ukikamilika mapema.

Wakulima hawako peke yao kwenye shauku ya kuona uwanja huo wa ndege; kwani wamo pia viongozi wakuu wa serikali, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida. Wote wanauangalia uwanja huo kama mkombozi wao; kwamba kukamilika kwake kutarahisisha na kuharakisha zaidi shughuli zao.

Wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Chuo cha Ualimu Uyole cha Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT), Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alielezea kwa mapana umuhimu wa uwanja huo kwa maendeleo ya ukanda huo wa Nyanda za Juu Kusini pamoja na taifa kwa ujumla.

Waziri Mkuu anasema kuwa tayari wafanyabiashara wakubwa kutoka Dubai wanapenda sana kuwekeza jijini Mbeya kwa kufungua vituo vyao (hub) ambavyo vitahudumia Ukanda wa Kusini mwa Afrika hivyo kuwapunguzia wafanyabiashara wa ukanda huo gharama na usumbufu wa kufuata bidhaa Dubai.

Lakini pamoja na kuweka vituo hivyo, Pinda anasema kuwa wafanyabiashara hao wamevutiwa na nyama kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, kwa hiyo wanakusudia vile vile kufanya biashara ya kusafirisha nyama kwenda kwao.

Mbali ya wafanyabiashara kutoka Dubai, Waziri Mkuu anawataja wafanyabiashara wengine wenye nia ya kufanya biashara na mikoa hiyo ya Rukwa, Mbeya, Iringa na Ruvuma kuwa ni wale wa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambao bidhaa kubwa waitakayo ni chakula.

Mbunge wa Jimbo la Mufindi, Joseph Mungai ni miongoni mwa viongozi wenye kusubiri kwa hamu kukamilika kwa uwanja huo ili usaidie kufungua soko kubwa la dunia la bidhaa za kilimo kwa wakulima wa mikoa hiyo.

Katika moja ya mazungumzo yake kuhusu uwanja huo, Mungai alitoa historia ya mikoa hiyo kuwa wazalishaji wakubwa wa maua enzi hizo za ukoloni, maua ambayo alisema ndiyo yaliyokuwa yakitumika kwenye Jumba la Malkia wa Uingereza, yakisafirishwa kila siku ya Ijumaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Mbeya hadi jijini London.

Ni wazi kwamba kukamilika wa uwanja huyo wa ndege kutasaidia sana kupanua soko la bidhaa za kilimo kutoka mikoa hiyo ya Nyanda za Juu Kusini maarufu kwa uzalishaji wa chakula hapa nchini.

Mratibu wa ujenzi wa Uwanja wa Songwe kutoka Kampuni ya Ujenzi ya Kundan Singh, Bw. Paul anabainisha kukamilika kwa uwanja huo katika wakati uliopangwa ambapo hivi sasa wako katika kukamilisha sehemu ya kurukia ndege.

Paul anasema kuchelewa kukamilika kwa uwanja huo kulichangiwa zaidi na mabadiliko yaliyofanywa kwenye michoro yake hivyo kusababisha kazi kuanza upya.

Anasema wakati michoro ya uwanja huo inabadilishwa, kwa upande wa sehemu ya kurukia ndege ilikuwa tayari imebaki tabaka moja tu la udongo na kisha ifuatiwe na tabaka la lami ili iwe imekamilika.

Miongoni mwa maeneo yaliyofanyiwa marekebisho ni pamoja na sehemu ya kutua na kurukia ndege ambayo hivi sasa imepanuliwa ambapo kazi yake hivi sasa imekamilika kwa asilimia 75 wakiwa katika hatua ya tabaka la mwisho la udongo na kisha waweke lami.

Uwanja wa Ndege wa Songwe unajengwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA) ambapo kazi rasmi za ujenzi zilianza mwaka 2004 kwa pesa na mkandarasi wa ndani, lakini baadaye Serikali ikawasiliana na Benki ya Maendeleo ya Uarabuni (BADEA) ambayo ilikubali kusaidia kukamilisha ujenzi wa uwanja huo.

Michoro ya awali ya ujenzi wa uwanja huo ilikuwa kwa ajili ya ndege za ukubwa wa Fokker F50 lakini baada ya ujenzi wa majengo na sehemu ya kurukia kuanza, michoro ilibadilishwa ili uwanja huo uweze kupokea ndege za ukubwa wa Boeing 737, kazi ambayo ndiyo inayoendelea kufanywa hivi sasa na Kampuni ya Kundan Singh kutoka nchini Kenya.

0 comments:

Post a Comment

 
BONYA HAPA