NEW DELHI:
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton akiwa ziarani nchini India amekutana na Waziri wa Mazingira Jairam Ramesh na maafisa waandamizi wa serikali ya India kujadili tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa. Baadae, Clinton aliwaambia waandishi wa habari kuwa sasa anaamini kuwa Marekani na India zitaweza kuandaa mpango utakaoleta mageuzi makubwa katika utaratibu wa uzalishaji,utumiaji na hifadhi ya nishati na wakati huo huo kuvutia uwekezaji mpya na kutoa nafasi za ajira kwa mamilioni ya watu.
Clinton, aliianza ziara yake nchini India siku ya Jumamosi katika mji mkuu wa kibiashara Mumbai ambako alikutana na viongozi wa biashara,wahanga wa mashambulizi ya kigaidi ya Novemba mwaka jana na wanaharakati wanawake.
Jumatatu, Clinton atakutana na Waziri Mkuu wa India Manmohan Singh na Waziri wa Mambo ya Nje SM Krishna. Mada kuu katika ajenda ya Clinton ni vita dhidi ya ugaidi, masuala ya nyuklia na tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa.

0 comments:
Post a Comment