
Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesema fedha zilizotolewa na serikali ili kusaidia wazalishaji wadogo wadogo, maarufu kama mamilioni ya JK, hazijawanufaisha masikini visiwani hapa kwa sababu wamekopeshwa wabunge na wakurugenzi.
Wawakilishi hao, waliyasema hayo wakati wakichangia Bajeti ya Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto kwa mwaka wa fedha 2009/10 katika kikao chao kinachoendelea mjini Unguja.
Mwakilishi wa jimbo la Kiwani, Hija Hassan Hija, alisema ana ushahidi wa fedha hizo kukopeshwa wabunge na Wakurugenzi na siyo walengwa kama ilivyokusudiwa na Rais Jakaya Kikwete.
Alisema wananchi waliopaswa kunufaika na fedha hizo wamekuwa wakitumia muda mwingi kuzifuatilia, lakini wengi hawajanufaika nazo.
Alisema kitendo hicho ni kinyume na misingi ya utawala bora na hivyo akaitaka serikali kuchukua hatua stahili ili walengwa wazipate.
Nae Mwakilishi wa Viti Maalum, Zakia Omar Juma alisema kwamba mifuko ya maendeleo inayoanzishwa na viongozi, lazima ilenge kuwainua akinamama wanaoishi katika mazingira magumu ya kimaisha.
Hata hivyo, aliitaka serikali itoe maelezo akinamama wa Zanzibar wamekuwa wakinufaika vipi na mfuko wa maendeleo ya wanawake ulioanzishwa na mke wa Rais, Mama Salma Kikwete na ule ulioanzishwa na Jumuiya ya Zayedesa, inayoongozwa na mke wa Rais Karume, Mama Shadya.
Alisema kwamba kuna akinamama wengi wanaishi katika mazingira magumu ya umasikini hasa katika Wilaya ya Micheweni Pemba, lakini hawaonekani kulengwa kuinuliwa kiuchumi na mifuko hiyo.
Mwakilishi wa Viti Maalum, Najma Khalfan alisema tatizo la vijana kuijiingiza katika vitendo vya ukahaba vinatokana na msukumo mdogo wa serikali katika kuwawezesha kupata ajira.
0 comments:
Post a Comment