Patricia Kimelemeta
MRADI wa chanjo ya kinga dhidi ya virusi vya ukimwi iliyotolewa nchini mwaka 2007 kwa askari polisi 60, imeonyesha kuwa na mafanikio katika awamu ya kwanza.
Chanjo hiyo inajulikana kitaalamu kama DNA-MVA Prime Boost, ilitolewa mwaka juzi na wataalamu wa afya wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba cha Muhimbili (Muhas) kwa kushirikiana na taasisi mbili za afya za nchini Sweden.
Taasisi hizo ni ile inayojishughulisha na Magonjwa ya Kuambukiza (SIIDC) na Chuo cha Karolinsika (KI) na mradi unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania pamoja na msaada kutoka Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Misaada la Sweden (SIDA).
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, Ofisa Habari wa Muhas, Hellen Mtui alisema kuwa mradi huo umeonyesha mafanikio makubwa na kwa sasa uko katika awamu ya pili.
Alisema lengo ni kuhakikisha kuwa wanatafuta kinga dhidi ya ugonjwa huo, ambao mpaka sasa hauna tiba ya uhakika iliyothibitishwa.
Mtui alisema askari waliofanyiwa chanjo hiyo, wanaendelea vizuri na hakuna hata mmoja ambaye ameonyesha kuambukizwa virusi vya Ukimwi.
Alisema tangu wapatiwe chanjo hiyo, askari hao hawajawahi kupata madhara yoyote yatokanayo na dawa walizofanyiwa, jambo ambalo limewasaidia kuingia katika awamu ya pili ya mradi wa chanjo hiyo mwaka huu.
``Sasa hivi tumeingia kwenye awamu ya pili ya mradi, na tumewatumia askari walewale ambao walipatiwa chanjo hiyo kwa mara ya kwanza mwaka juzi.
``Lakini mpaka sasa hakuna hata mtu mmoja kati yao ambaye amelalamika kupata matatizo au usumbufu kuhusiana na dawa walizopatiwa, jambo ambalo tunaona tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika mradi wetu,`` alisema Mtui.
Mtui alisema kuwa kutokana na hali hiyo wanaamini kuwa katika awamu zote nne zitakapokwisha, watu hao wataweza kuwa na kinga nzuri ambayo itaweza kupigana na vijidudu vya aina zote, kwa sababu wanakuwa wamejitengenezea kinga bora kwenye majaribio hayo.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa awali na majaribio ya chanjo hiyo, yataiwezesha Tanzania kujenga uwezo wa kushiriki kikamilifu katika tafiti za namna hiyo ili hatimaye dunia iweze kupata chanjo muafaka dhidi ya VVU na inayokidhi aina ya virusi vilivyo hapa nchini.
Alisema watakaoshiriki katika utafiti wa chanjo hiyo ya majaribio, ni askari wa Jeshi la Polisi ambao wamejitolea kwa hiari yao.
Profesa Kisali Pallangyo, alikaririwa akisema kuwa utafiti wa chanjo hiyo ni matokeo ya ushirikiano wa muda mrefu (tangu mwaka 1986) kati ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi za Afya Muhimbili na taasisi mbili za nchini Sweden.
Profesa Pallangyo ambaye ni mmoja wa wataalamu wa mradi huo, alisema lengo la mradi huo ni kubaini usalama na uwezo wa dawa hiyo ya chanjo katika kutengeneza vichocheo vya kinga dhidi ya virusi vya Ukimwi katika mwili wa binadamu.
Katika utafiti wa awali uliofanyika nchini Sweden, Profesa Pallangyo alisema ilionyesha kuwa chanjo hiyo ni salama na kwamba ilikuwa na uwezo mzuri sana wa kutengeneza vichocheo vya kinga dhidi ya virusi vya Ukimwi.
0 comments:
Post a Comment