
Katika hali ambayo si ya kawaida kwa hapa kwetu Tanzania, wanafunzi wapatao 14 wamefunga ndoa huko Visiwani Zanzibar.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman ndiye aliyetoa taarifa hiyo jana.
Akasema wanafunzi hao walioana wao kwa wao msimu uliopita.
Waziri amesema hayo alipokuwa akisoma bajeti ya Wizara hiyo katika mwaka wa fedha wa 2009/2010 katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichofanyika mjini Zanzibar .
Akasema tatizo la mimba bado linaendelea kujitokeza Visiwani na kuitaka jamii kushirikiana na Serikali kudhibiti vitendo hivyo kwa vile vinavuruga maendeleo ya wanafunzi ambao ni taifa la kesho.
Kadhalika Waziri amesema katika mwaka uliopita, kesi 44 za ujauzito zilipokelewa ambapo kati ya hizo, 14 zilikuwa zikiwahusisha wanafunzi kwa wanafunzi kupeana mimba
Hata hivyo amesema wanafunzi waliohusika na sakata hilo wote walifukuzwa shule kwa vile kitendo hicho hakiwaruhusu kuendelea na masomo kwa mujibu wa sheria.
“ Mheshimiwa Spika, kati ya kesi zilizopokelewa, 14 ziliwahusisha wanafunzi kwa wanafunzi” akasema Waziri huyo.
Hata hivyo Waziri alisema mpango wa kutoa elimu mbadala umeshaanza utekelezaji wake Zanzibar ili kuwawezesha wanafunzi walioshindwa kuendelea na masomo kupata elimu ya ufundi
Alifafanua kuwa katika mwaka uliopita, wanafunzi 61 waliweza kuingia katika mpango huo na wanaendelea kupatiwa mafunzo ya ufundi ikiwemo ufundi seremala, ushonaji. Alisema jumla ya wanafunzi 41 walihitimu mafunzo yao kwa mwaka uliopita.
Akasema sheria inawaruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kwa bahati mbaya, kama vile kubakwa au mazingira yasiyokuwa rasmi kuendelea na madarasa ya elimu mbadala lakini sio kwa wanafunzi waliobeba ujauzito kwa hiari yao.
Waziri Haroun ameliomba Baraza la Wawakilishi kumuidhinishia jumla ya Sh. Bilioni 37.2.
0 comments:
Post a Comment