AFISA ubalozi wa Canada aliyekamatwa na polisi Kanda maalum ya Dar es salaam kwa tuhuma za kumtemea mate askari wa usalama barabarni mwenye namba E 1653 koplo Samson, amegoma kuhojiwa.
Jean Touchatte (48) ambaye ni katibu muhtasi wa ubalozi huo nchini alikamatwa juzi saa 8:15 mchana maeneo ya Banana jijini Dar es Salaam baada ya kumtemea mate askari huyo akiwa kazini.
Kaimu Kamanda wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Charles Kenyela aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa afisa huyo amegoma kutoa maelezo polisi akishinikiza kwanza awepo balozi wake.
Alisema siku ya tukio mtuhumiwa huyo ambaye ni katibu muhtasi wa ubalozini hapo, alimtemea mate koplo Samson wakati akiongoza magari yanayotoka Ukonga kuelekea Uwanja wa ndege.
Kamanda Kenyela alisema sababu za kumtemea mate askari huyo bado hazijajulikana na mtuhumiwa anashikiliwa kwa uchunguzi zaidi.
Alisema baada ya Koplo Samson kutoa taarifa polisi gari hilo lilitangazwa askari waliokuwa doria walioanza kulifuatilia na alipofika barabara ya Nyerere karibu na Kamata gari hilo lilikamatwa na kupelekwa Makao Makuu ya Polisi trafiki Kanda maalum ya Dar es salaam.
Kamanda Kenyela alisema wakati mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa walifika waandishi wa habari akiwemo Jerry Muro wa TBC kutaka kujua kwa nini katibu huyo alimtemea mate askari.
Wakati Jerry anamhoji naye alitemewa mate sehemu ya chini ya kidevu chake na kusambaa katika fulana yake aliyokuwa amevaa kitendo kilichosababisha mwandishi huyo kufungua jalada la shambulio CD/IR/4818/2009.
Kamanda Kenyela alisema fulana yenye mate imehifadhiwa kituo cha polisi kati wakati upelelezi unaendelea na kuongeza kuwa maelezo mengine kuhusiana na tukio hilo yatatolewa na Ispekta Jeneral wa Polisi Said Mwema.
Awali Kamanda wa kikosi cha Usalama Barabarani, James Kombe, alisema suala hilo walimuachia Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema, ungawa kwa mujibu wa taratibu atafikishwa mahakamani kulingana na uzito wa kosa linalomkabili.
Kombe alisema iwapo kosa lake litaonekana kuwa zito ataondolewa ulinzi wake na huenda hatimaye kufukuzwa nchini na kuwahakikishia wananchi kuwa haki itatendeka.
“Kwa mujibu wa taratibu huenda akafungiliwa mashitaka kuangalia uzito wa kosa alilofanya, iwapo kosa lake litaonekana kuwa zito ataondolewa kinga yake na kurudi nyumbani†alisema Kombe na kuongeza:
“Kwa kweli kitendo alichofanya ni kuidhalilisha nchi, hivyo naomba niwahakikishie wananchi kuwa haki itatendeka, na tayari huyo afisa yuko mikononi mwa polisi.â€
0 comments:
Post a Comment