Na Zaina Malongo
KATIKA kuhakikisha kwamba maisha ya Watanzania yanaboreshwa, Vodacom Tanzania kwa kushirikiana na kampuni ya usambazaji wa maji jijini, Dawasco, imeanzisha huduma ya bure kulipia ankara zao kwa kupitia huduma ya Vodafone M-PESA.
Akizungumza hivi karibuni Makao Makuu ya Dawasco wakati wa hafla ya makubaliano ya kutoa huduma hiyo, Mkurugenzi wa Masoko wa Vodacom Tanzania Ephraim Mafuru alisema huduma hiyo ni ubunifu mwingine wa Vodacom unaolenga kuboresha maisha ya wateja wake.
Alisema kupitia huduma hiyo, wateja wa Vodacom Tanzania, wanaweza kulipa ankara zao za maji viganjani mwao kwa kutumia simu zao za mkononi badala ya kupanga foleni ndefu kwa lengo la kulipa ankara zao.
“Haya mapinduzi makubwa yanayoletwa na Vodacom Tanzania, mtandao unaoongoza hapa nchini, wateja wetu wategemee makubwa zaidi,” alisema Mafuru.
Alisema Vodacom Tanzania inapenda kuwakaribisha DAWASCO katika ulimwengu wa Vodafone M-Pesa na kwamba, anafarijika kuona kwamba wadau mbalimbali wanashirikiana na Vodacom kufanikisha huduma mbalimbali kwa umma.
Mwaka jana mwezi Aprili, Vodacom Tanzania, ilizindua rasmi huduma yake ya kutuma pesa kwa kutumia simu za mkononi ijulikanayo kama Vodafone M-Pesa. Huduma inayotolewa na mtandao wa Vodacom kwa kushirikiana na kundi la Vodafone.
Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo, ndiye aliyeizindua rasmi huduma hiyo na aliipongeza Vodacom kwa kuanzisha huduma hiyo muhimu hapa nchini.
Naye Afisa Biashara wa Dawasco, Raymond Mndolwa, aliipongeza Vodacom kwa ushirikiano huo ambao pia unalenga katika kuboresha huduma za Dawasco.
Kumbuka mitandao ya Vodacom inapatikana ndani na nje ya nchi yetu, kwa hiyo haijalishi kama uko hapa Tanzania au nje ya nchi, bado unaweza kulipia ankara yako popote na Vodafone M-Pesa.
0 comments:
Post a Comment