Baada ya serikali kusitisha uamuzi wake wa kuzifutia taasisi za dini na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) misamaha ya kodi, sasa imeagiza mashirika hayo kufuatiliwa.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeagizwa kutafiti misamaha ya kodi inayoitoa kwa madhehebu ya dini na NGOs, kwa lengo kudhibiti matumizi mabaya ya misaada hiyo.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mukulo, mwishoni mwa wiki mjini hapa wakati akizungumza na wafanyakazi wa TRA mkoani hapa kwenye ukumbi wa mikutano wa jengo la mamlaka hiyo wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Mkulo alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kubaini waombaji wanaotumia misamaha hiyo kujinufaisha wao binafsi, hivyo kuikosesha serikali mapato kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Waziri huyo alisema uzoefu unaonyesha kuna baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vibaya misamaha ya kodi kwa kuingiza vifaa mbalimbali, na mali zingine bila kulipa kodi, hivyo kuikosesha serikali mapato.
Akiwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2009/10 bungeni Juni 11, mwaka huu, Mkulo alitangaza uamuzi wa serikali wa kufuta misamaha ya Kodi la Ongezeko la Thamani (VAT) kwa mashirika ya dini na NGOs kwa maelezo kuwa baadhi ya taasisi hizo zimekuwa zikiitumia vibaya misamaha hiyo.
Uamuzi huo wa serikali ulipingwa vikali na viongozi wa taasisi za dini, ambao walisema utawazuia kama wadau wa maendeleo kutoa misaada kwa jamii hususan huduma za afya, elimu na miundombinu.
Shinikizo hilo liliilazimisha serikali kusitisha uamuzi huo baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kukutana na viongozi wa taasisi za dini mjini Dodoma na kukubaliana kuunda kamati ya pamoja ya kufuatilia na kuhakikisha kuwa misamaha hiyo haitumiki vibaya.
Mbali na uamuzi huo kupingwa na taasisi za dini, lakini pia wabunge kadhaa waliochangia hotuba ya bajeti waliishauri serikali kusitisha hatua hiyo kwa hoja kwamba inasababisha kuzorota kwa huduma za jamii kutokana na taasisi hizo kutoa mchango mkubwa.
Aidha, Waziri Mkulo ameagiza kubana mianya yote inayopitisha bidhaa mbalimbali ili kuiongezea serikali mapato.
Meneja wa TRA Mkoa wa Singida, Jumbe Samson, alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2008/2009, wamekusanya mapato ya zaidi ya Sh. bilioni 1.4.
Kwa mujibu wa Samson, kiasi hicho ni sawa na asilimia 79.4 ya lengo lililokusudiwa la kukusanya Sh. 1,797,700,000 walizopangiwa na Makao Makuu ya TRA.
0 comments:
Post a Comment