TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU / ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT CHEAP RATES | CONTACT ME: kilinyepesi@gmail.com

 photo DTB_zps7bd2662d.jpg

 photo fl_zps09337f7a.jpg


Habari Mpya:
Friday, July 31, 2009

Serikali yatoa kauli mkataba kati ya Tanzania na Canada

3:04 PM

Serikali imetoa kauli yake kuhusu majadiliano ya mkataba wa Kukuza na Kulinda Vitega Uchumi kati ya Serikali ya Tanzania na ya Canada na kukanusha kwamba hauhusiani na suala la Tume ya Jaji Bomani iliyoundwa kushughulikia mapungufu katika sekta ya madini nchini.

Kauli hiyo ya Serikali ilitolewa jana bungeni na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo.

Hatua hiyo inafuatia swali la Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alilomuuliza Waziri Mkuu Alhamisi ya wiki iliyopita, Julai 23, katika kipindi cha maswali ya papo kwa pao.

Kabwe alitaka kupata maelezo kutoka kwa Waziri Mkuu kwamba ni kwa nini taarifa ya Tume ya Jaji Bomani haijatungiwa sheria ili makampuni ya Canada na hasa katika sekta ya madini na mengineyo yaendelee kufaidika na utajiri uliopo nchini wa madini na kwamba Serikali ya Tanzania haijatoa taarifa kuhusu mkataba huo kwa umma ingawa majadiliano yanaendelea.

Akitoa kauli ya serikali, Mkulo alisema majadiliano ya mkataba wa kukuza na kulinda vitega uchumi kati ya Tanzania na Canada na Tume ya Jaji Bomani iliyoundwa kushughulikia mapungufu katika sekta ya madini nchini ni masuala mawili tofauti.

Alisema wakati Tume ya Jaji Bomani ilipewa jukumu la kudurusu mikataba na kuainisha mapungufu katika uwekezaji kwenye sekta ya madini, rasimu ya mkataba baina ya kukuza na kulinda vitega uchumi inaangalia masuala yanayohusu sekta zote za uwekezaji na kulinda vitega uchumi kwa jumla baina ya nchi zote mbili.

Alisema mchakato huo wa majadiliano baina ya nchi hizo mbili ulianza mwanzoni mwa mwaka 2004 na kufuatiwa na majadiliano yasiyo rasmi ya Novemba 5 na 6 mwaka 2007 ambapo awamu ya kwanza yalifanyika Ottawa nchini Canada mwaka 2008 na kufuatiwa na ya tatu ya Septemba 15 hadi 19 mwaka huo huo wa 2008.

Mkulo alifafanua kuwa hadi kumalizika kwa majadiliano ya tatu, pande zote mbili bado hazijakubaliana kwenye vipengele vingi vya rasimu ya mkataba na hivi sasa kamati ya majadiliano inapitia mapendekezo mapya yaliwasilishwa na Serikali ya Canada kuhusu rasimu ya mkataba husika kabla ya kuanza tena majadiliano ya awamu ya nne.

Alibainisha kuwa chimbuko la majadiliano hayo ni baada ya Tanzania kuridhia mikataba iliyoanzishwa na ‘Multilateral Investment Guarantee Agency (MIGA)’ pamoja na ile ya ‘International Centre for Settlement of Investment Disputes (ICSID)’ kuwa migogoro inayotokana na vitega uchumi vilivyoelekezwa na wawekezaji iwe inasuluhishwa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na kukubaliwa kimataifa.

Mkulo alivitaja vipengele muhimu vinavyozingatiwa katika makubaliano na nchi mbalimbali kuhusu mikataba hiyo kwamba ni pamoja na uendelezaji wa uwekezaji rasilimali, ulinzi wa vitega uchumi, utoaji wa vivutio kwa wawekezaji, utaifishaji wa rasilimali, fidia wakati wa matukio yasiyokuwa ya kawaida kama vile vita na machafuko.

Vipengele vingine alisema ni pamoja na uhamasishaji mali na faida, usuluhishi wa migogoro na utaratibu wa muda wa kuanza utekelezaji wa makubaliano.

Kwa mujibu wa Waziri, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa maslahi ya Taifa yanalindwa na pia mikataba hiyo inalenga kuwajengea imani na uhakika wawekezaji kutoka nje kwamba vitega uchumi vyao vitakuwa salama nchini Tanzania kama sera ya kukuza uwekezaji ya mwaka 1996 inavyoelekeza.

Tanzania ina mikataba ya aina hiyo na kwamba tayari inatekelezwa baina ya nchi za Uingereza, Sweden, Denmark, Finland, Italia, Uholanzi, Uswisi, Afrika ya Kusini na Mauritius

0 comments:

Post a Comment

 
BONYA HAPA