
Mjadala wa waraka wa Kanisa Katoliki ulioandaliwa kutoa elimu ya uraia kwa waumini wake kwa ajIli ya uchaguzi mkuu mwakani, umeibuka tena bungeni, hali iliyomfanya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuliomba kanisa kutopuuza maoni yanayotolewa juu yake.
Pinda alilazimika kutoa kauli hiyo jana wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, kufuatia swali la Mbunge wa Chambani (CUF), Salim Hemed Khamis.
Khamis alitaka kujua msimamo wa serikali kuhusu waraka uliotolewa na kanisa hilo ambao hivi karibuni kumekuwa kukitolewa maoni mbalimbali na wanasiasa, wakiwemo wabunge, viongozi wa kidini na wananchi mbalimbali.
Pinda alisema sio mara ya kwanza kwa kanisa hilo kutoa waraka kama huo kwani walikwisha kufanya hivyo mara mbili huko nyuma, lakini hakukuwa na malalamiko kama ya safari hii.
“Sasa ninachoweza kusema mimi ni nini? Mimi si mara ya kwanza kuona ilani karibu kila wakati wa uchaguzi unapokaribia wamekuwa wakifanya hivyo. Lakini lazima tukubali vile vile kwamba mambo haya yanakwenda na wakati,” alisema. “Mara ya kwanza sikusikia maneno juu ya jambo hili yaani katika uchaguzi ule wa kwanza, lakini hata ule wa pili, lakini safari hii yamejitokeza,” alisema.
“Dhehebu hili ambalo wametoa jambo hili wasipuuze kauli za Watanzania zinazojitokeza sasa, na mimi nadhani kubwa hapa ni kwamba je, hivi kama kila dhehebu litaamua kutoa ilani yake tutakuwa na uwezo wa kudhibiti yale yaliyomo katika hizo ilani?” Alihoji na kuongeza: “Maana ndio wasiwasi wangu.”
“Kwa hiyo, upande wa serikali ni lazima vile vile waanze kufikiria kwamba pengine iko haja ya kuzungumza na madhehebu ya dini hata kama inabidi yatoe maelekezo fulani, pengine iko haja ya kusema hivi hamuwezi hayo mawazo yenu mkayaleta serikalini halafu yakatoka kwa mfumo mmoja kama yana nia nzuri ambayo hatuna uhakika kama yanasaidia kujenga umoja wa kitaifa au yanaweza yakapelekea kubomoka kwa umoja wa kitaifa,” alisema.
Alisema baada ya kusikiliza majadiliano marefu sana anadhani Wakatoliki wamesikia na akatoa rai kwamba wasipuuze kwani mengine ni majadiliano mazuri tu ya kujaribu kusema wanachohitaji watu.
“Sasa upande wa serikali tutaangalia tuone na sisi tunajipangaje na tufanye nini ili kuhakikisha umoja wa kitaifa unaendelea kuwepo maana ndiyo kazi kubwa tuliyonayo,” alisema.
Baada ya majibu hayo, Khamis aliuliza swali lingine la nyongeza, ambapo alianza na maelezo kwamba yanapotolewa matamko mazito kama haya ambayo yanagusa hisia za watu wengi, serikali inaonekana kuchelewa kuyatolea maelezo kama alivyofanya kwa ujasiri mkubwa Mbunge wa Kuteuliwa, Kingunge Ngombale Mwiru.
Ndipo akauliza: “Je, mheshimiwa Waziri Mkuu, huoni kama hii inakaribisha machafuko ya hali ya hewa kisiasa nchini wakati imechelewa na watu wanaendelea kubishana na kubishana?"
Katika majibu yake, Waziri Mkuu Pinda alisema: “Haraka haraka nayo haina baraka, wakati mwingine si vizuri ukaharakisha kuingilia kati wakati hujapata hasa tatizo likoje.”
Alisema yeye ana hakika kabisa kwamba baada ya mazungumzo marefu na mabishano ambayo yalikuwa yakiendelea, wako katika nafasi nzuri zaidi kama serikali kuona busara ipi sasa itumike katika kujaribu kuelekeza taifa na watu wake katika masuala kama haya.
“Kwa hiyo, mimi nadhani hatujakosea na wala sidhani tumefikia mahali ambapo nafikiri mchafuko wa hali ya hewa utajitokeza kwa sababu ya jambo hili, hapana. Mimi nadhani bado yako ndani ya uwezo wetu kuweza kulisimamia vizuri,” alisema Pinda
Mjadala kuhusu waraka ulioandaliwa na Kanisa Katoliki kwa ajili ya kuwapa waumini wake elimu ya uraia, uliibuka baada ya Kingunge kulitaka Kanisa hilo kuuondoa kwa maelezo kuwa unaweza kuwagawa Watanzania na kubomoa umoja wa kitaifa.
Kingunge alitoa madai hayo wakati akijadili hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kwa mwaka 2009/10 iliyowasilishwa na waziri wa wizara hiyo, George Mkuchika.
Kutokana na kauli ya Kingunge, viongozi mbalimbali wa Katoliki nchini walimpuuza Kingunge na kumtaka aeleze sehemu yoyote ya waraka huo yenye matatizo kuliko kujikita katika kauli za kiujumla tu. Pia, baadhi walisema Kingunge alikuwa hajausoma waraka huo, huku watu wengine wakisema kwamba wanaoogopa waraka huo ni wakala wa mafisadi kwa kuwa unahimiza kuchaguliwa viongozi waadilifu.
0 comments:
Post a Comment