TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU / ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT CHEAP RATES | CONTACT ME: kilinyepesi@gmail.com

 photo DTB_zps7bd2662d.jpg

 photo fl_zps09337f7a.jpg


Habari Mpya:
Tuesday, July 28, 2009

Mafua ya nguruwe yarejea Dar wazungu wawili wagundulika uwanja wa ndege

11:45 PM
Hussein Issa na Glory Kimath

WIKI tatu baada ya mgonjwa wa kwanza wa homa ya mafua ya nguruwe raia wa Uingereza kugundulika Dar es Salama, wagonjwa wengine wawili raia wa nchi hiyo wamegundulika kuwa nao na kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu.

Raia hao ambao ni ndugu wa familia moja, wanaoishi Mbezi Beach jijini, walibainika kuwa na ugonjwa huo Jumapili iliyopita katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere wakati wakirejea kutoka Nairobi, Kenya walikokwenda kukutana na ndugu zao.

Baada ya kubainika kuwa na ugonjwa huo walipelekwa moja kwa moja Muhimbili ambako wamelazwa kwa ajili ya matibabu.

Mgonjwa wa kwanza hapa nchini aligundulika Julai 4, mwaka huu katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakati akiingia nchini kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.

Taarifa ya Wizara ya Afya ilisema raia huyo wa Uingereza alitoka London na kutua Nairobi, Kenya kabla ya kuingia nchini.

Mkurugenzi wa Huduma ya Tiba wa MNH, Profesa Andrew Swai alithibitisha jana kuwepo kwa wagonjwa hao katika hospitali hiyo, lakini alikataa kutaja majina yao kwa maelezo kwamba, kufanya hivyo ni kinyume cha maadili ya kazi yao.

"Hawa kina dada ambao nadhani ni ndugu ni raia wa Uingereza, walitokea Kenya katika mkutano na ndugu zao wanaoishi huko; ila sio vizuri kuwataja majina kwani kisheria tukiwataja ni kuwadhalilisha na wakitoka watu watawasumbua," alisema Profesa Swai.

Aliongeza kuwa majina yao hayana faida kwa jamii, ila kinachotakiwa ni kufahamika kuwa ugonjwa huo upo na wananchi wawe makini sana, hususan wanaokwenda nje ya nchi na wanaoishi mpakani, ili wasipate maambukizo.

Profesa Swai, alisema wagonjwa hao waliletwa siku ya Julai 26 mwaka huu hospitalini Muhimbili wakitokea uwanja wa ndege wa kimataifa, Julius Nyerere.

"Unajua tumejizatiti kukabiliana na ugonjwa huo kila kona, kuanzia katika mipaka ya kuingia nchini, bandarini na viwanja vya ndege vilivyopo nchini; hivyo ilikuwa rahisi kuwatambua wagonjwa hao," alisema Profesa Swai.

Hata hivyo alifahamisha kuwa wagonjwa hao wanaendelea vizuri na matibabu na kwamba, muda wowote wanaweza kuruhusiwa kwenda nyumbani kwao.

Gazeti hili lilipata taarifa za kuwepo kwa wagonjwa hao tangu juzi na lilipofika Muhimbili kupata ukweli na ufafanuzi wake, maafisa uhusiano wa Muhimbili hawakusema lolote.

Chanzo cha taarifa hizo kililiambia gazeti hili kuwa wagonjwa hao ambao ni ndugu walipelekwa hospitalini hapo kwa gari la wagonjwa la Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere juzi majira ya saa kumi jioni.

Kilifahamisha kuwa wagonjwa hao wamelazwa katika chumba maalumu katika hospitali hiyo, kinachojulikana na baadhi ya wauguzi, ili habari za kuwepo kwa wagonjwa hao nchini zisienee kwa wananchi na hatimaye kuwatia hofu.

“Unaona wamelazwa katika vyumba vile, lakini hutakiwi kusogea pale kwani watakushangaa wewe ni nani na pia usalama wako kiafya utakuwa hatarini, kuambukizwa ugonjwa huo,” kilisema chanzo chetu hospitalini hapo na kuongeza:

“Viongozi wa hospitali wanafanya siri, hata sisi na wauguzi wengine hatutakiwi tufahamu kwa madai kwamba, tutatoa taarifa kwa wananchi na hatimaye kuwatia hofu”.

Awali, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Aisha Kigoda alisema wananchi wanatakiwa kuwa makini na ugonjwa huo na kutoa taarifa mara wanapoona mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.

Katika harakati za kukabiliana na ugonjwa huo, mwezi uliopita Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa alisema serikali imejizatiti kikamilifu kwa kuweka wataalamu wake mpakani, bandarini na viwanja vya ndege ambako huwapima watu wote wanaingia nchini kutoka nje.

Ugonjwa huo ambao dalili zake ni pamoja na homa ya ghafla, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo, misuli na uchovu wa mwili umekuwa tishio duniani kote, lakini kwa nchi za Afrika wanaogundulika kuwa nao wengi wao ni wageni wanaotoka nchi za Ulaya.

Dalili nyingine za ugonjwa huo ni pamoja na kikohozi, mafua, maumivu yakoo, kichefuchefu, kusikia dalili za mwili kutetemeka na kukosa hamu ya kula chakula.

Wataalamu pia wanasema kwamba, wakati mwingine mgonjwa anaweza kuharisha na kutapika na kwamba wagonjwa wengine huzidiwa na kupata vichomi pamoja na kushindwa kupumua vizuri.

Wagonjwa wa kwanza wa homa ya mafua ya nguruwe waligundulika nchini Mexico Machi, mwaka huu na baadaye Marekani, kisha nchi za Ulaya. Afrika Msahariki na hasa Kenya waliwagunduka Juni wengi wao wakiwa wageni kutoka Ulaya.



0 comments:

Post a Comment

 
BONYA HAPA