
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limemkana askari wake, koplo Julius Abraham Kwayu, ambaye alidaiwa kuhusika katika tukio la ujambazi lililotokea Julai 24 mwaka huu, Manzese jijini Dar es Salaam na kueleza kwamba aliomba likizo na hakurejea kwa muda mrefu.
Taarifa ya JWTZ iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano makao makuu ya Jeshi hilo kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana ilisema Koplo Kwayu, alikuwa mtoro wa jeshi kwa kipindi kirefu na kwamba jeshi lilikuwa likimtafuta.
JWTZ katika taarifa hiyo, limempongeza Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na kikosi chake kwa kufanikisha kuwatia mbaroni majambazi hao.
"JWTZ, Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wanashirikiana kwa karibu kufuatilia mwenendo wa watumishi wasiokuwa waaminifu kama ilivyojitokeza kwa Koplo Julius Abraham katika matukio mengine kama hayo ya ujambazi," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilifafanua kuwa ili kukabiliana na tabia mbaya kwa baadhi ya watumishi, jeshi limebadili utaratibu wa kuajiri askari wapya na kwamba kuanzia sasa vijana wote wanaoomba kujiunga na JWTZ watalazimika kupata mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) au Jeshi la kujenga Uchumi (JKU) ili wachunguzwe mienendo yao.
0 comments:
Post a Comment