TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU / ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT CHEAP RATES | CONTACT ME: kilinyepesi@gmail.com

 photo DTB_zps7bd2662d.jpg

 photo fl_zps09337f7a.jpg


Habari Mpya:
Tuesday, July 28, 2009

Dk. Mwakyembe ailipua Barrick

2:45 PM

Mbunge wa Kyela (CCM), Dk. Harrison Mwakyembe, amependekeza kufungwa kwa mgodi wa dhahabu wa North Mara, unaomilikiwa na kampuni ya kimataifa ya uchimbaji madini ya Barrick Ltd kutokana na tuhuma za uchafuzi wa sumu katika maji ya mto Tigithe, ambapo watu kadhaa wamedaiwa kufa na wengine kuathirika.

Dk. Mwakyembe alisema hayo jana wakati akichangia hotuba ya makadirio ya matumizi ya fedha ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2009/10, iliyowasilishwa bungeni mwishoni mwa wiki na waziri wake, Wiliam Ngeleja.

“Pamoja na mapenzi mengi kwa wawekezaji, safari hii lazima tuchukue hatua dhidi ya mgodi wa North Mara, tufunge mgodi wa North Mara mpaka hatua itakapochukuliwa ya kurekebisha mfumo wake wa taka ya sumu,” alisema.

Alitaja hatua nyingine kuwa ni kuweka mpaka kati ya eneo la mgodi na makazi ya wananchi.

Dk. Mwakyembe alisema hatua kama hiyo pia ichukuliwe kwa

mgodi wa dhahabu wa Geita, uliopo mkoani Mwanza kwa kumwaga sumu kwa wananchi. Aliwataka wabunge wanaotoka maeneo hayo pamoja na wanasheria na wanaharakati kuwahamasisha wenzao kuifikisha mahakamani kampuni ya Barrick, kwa kuhatarisha maisha ya wakazi wanaozunguka migodi yao.

Alisema hatua hiyo itakuwa ni mwafaka kwao kwani haitatosha kupiga kelele majukwaani.

Baada ya kilio cha wakazi wa North Mara kuhusu uchafuzi wa maji yao, Bunge liliteua Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira chini ya Mwenyekiti wake, Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai (CCM), kwenda kufanya uchunguzi huo. Timu hiyo pia iliwahusisha wabunge wa Kamati ya Nishati na madini.

Ripoti hiyo imekwishakabidhiwa kwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, lakini bado haijapangiwa ratiba ya kusomwa bungeni na wabunge kupata nafasi ya kuijadili.

Dk. Mwakyembe alisema kampuni ya Barrick inasifika duniani kwa uchafuzi wa mazingira na akaitaja Norway kuwa ni moja ya nchi ambayo iliifukuza kampuni hiyo nchini humo.

Katika hatua nyingine, Dk. Mwakyembe alitaka misamaha ya kodi kwa wawekezaji wa madini ifutwe na tena kwa makampuni yote, na akahoji ni kwanini wawekezaji kama hawa wanaogopwa.

Alitaka ununuzi wa mafuta nchini ufanywe kwa pamoja ili kuachana na utaratibu wa kuagiza mafuta kwa mtu mmoja mmoja, utaratibu ambao unachangia ongezeko la bei ya mafuta kwa wateja. Alisema utaratibu wa kuagiza mafuta kwa pamoja unatumika katika nchi za Malawi na Zambia na bei ya mafuta katika nchi hizo ni ndogo au inalingana na ile ya hapa.

Kama hiyo nayo haikutosha, Dk. Mwakyembe aliishukia Mamlaka ya Udhibiti wa Matumizi ya Nishati na Maji (Ewura), kwa kushindwa kuwadhibiti watu wanaochanganya mafuta ya taa na diezeli kwa manufaa yao ya kibiashara. Alisema Ewura inawafahamu wahusika hao na maeneo maarufu ya kuchakachua mafuta ambayo aliyataja kuwa ni kuanzia Kibaha hadi Chalinze, lakini mamlaka hiyo imeshindwa kuchukua hatua yoyote. Alisema anaipa Ewura muda wa miezi mitatu kufanya kazi na kama watashindwa atawasilisha bungeni hoja binafsi dhidi ya mamlaka hiyo. “Ewura tunawapa miezi mitatu, na mimi nitakuja na hoja hapa kuwataka Ewura wafanye kazi la sivyo waondoke, kama ni mshiko unawasumbua wafumbue macho,” alisema. Akizungumzia madini ya uranium yaliyogunduliwa nchini hivi karibuni, Dk. Mwakyembe alionyesha wasiwasi wake iwapo taifa limejiandaa vema kuchimba au hata katika kuweka mikabata mizuri ili uchimbaji utakapoanza uwanufaishe wananchi.

Alisema Tanzania sio nchi pekee katika Afrika kugundua kuwa ina madini hayo, kwani yameguliwa pia katika nchi nyingine 18 na akaitaka serikali kujifunza kutoka kwa nchi nyingine ambazo tayari zimeanza uchimbaji ili kuona namna gani madini hayo yanawanufaisha wananchi na mataifa yao kwa ujumla.

Alitaja baadhi ya nchi hizo kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Malawi na Uganda, ambazo Tanzania inaweza kujifunza na kisha kuamua namna bora zaidi ya kunufaika na madini hayo.

Alisema kama mambo hayo yatakuwa bado ni heri madini hayo yakaachwa kama ambavyo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alivyowahi kukataa kuchimbwa kwa madini kwa sababu taifa lilikuwa bado halijajiandaa. “Hizi ni habari njema, lakini natoa angalizo, ikiwa sisi viongozi tutaweka maslahi yetu mbele mbele na kuendekeza umimi katika uchimbaji wa madini hayo, tutazalisha ma Richmond na EPA wengine na kisha kusafishana kama tunavyofanya sasa,” alisema na kuongeza: “Ni heri madini hayo yaendelee kubaki ardhini.”

“Nyerere na Karume (Rais wa kwanza wa Zanzibar Aman Karume), walitaka madini yetu yasichimbwe, leo tunachimba sisi, lakini wanaofaidika ni nani. Tunashuhudia tunavyotoana macho sasa,” alisema.

Katika hatua nyingine, Dk. Mwakyembe aliishukuru serikali kwa uamuzi wa kuurudisha serikalini mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, lakini akaomba wafanyakazi wa mgodi huo ambao hawajalipwa kwa miezi mingi sasa serikali iangalie namna ya kuwalipa.


0 comments:

Post a Comment

 
BONYA HAPA